
CHAMA cha CUF kimemtaka Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad
kutafuta chama kingine kama hawezi kufanya kazi na Mwenyekiti, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama
hicho, Abdul Kambaya alimsihi Maalim kutambua kuwa CUF si kampuni yake
bali chama cha siasa, hivyo hana mamlaka ya kuwachagulia wanachama
mwenyekiti.
Alisema ni muhimu Maalim Seif akatambua kwamba wahuni ni wanaofanya kazi
za chama hicho kwenye hoteli na mitandao ya kijamii na viongozi halali
wa kitaifa wa CUF wako ofisi za Buguruni.
“Anapaswa kutambua kuwa CUF ni taasisi, ni chama cha siasa, si kampuni
yake, wala si mali yake, hivyo hana uamuzi na hawezi kutuchagulia
kiongozi. Yeye na Mwenyekiti wamechaguliwa na Mkutano Mkuu, kwa hiyo
kama anasema hawezi kufanya kazi na Mwenyekiti wake, atafute pa kwenda
yeye na wapambe wake,” alisema.
Akifafanua masuala yaliyozungumzwa na Maalim Seif juzi, ambaye alimtaja
kwa jina Sultan wa Pili wa Zanzibar, alisema kuhusu vyombo vya Dola
kumzuia kufanya ziara Lindi na Mtwara mwishoni mwa mwaka wa jana, jambo
hilo alishalizungumza na makamanda wa Polisi wa mikoa ya Mtwara na
Lindi nao walishaeleza sababu za uamuzi huo.
Alisema kimsingi kwenye jambo hilo palikuwa na ukiukwaji wa Seif
mwenyewe alipomtumia Katibu wa Jumuiya ya Vijana kumwandalia ziara hiyo
badala ya kutumia viongozi wa wilaya ya Mtwara Mjini.
Alifafanua kwamba jambo hilo lilifanya viongozi hao wa wilaya kujiona
wamedharaulika na kuamua kulijulisha Jeshi la Polisi kuwa hawana taarifa
ya ziara hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi lilikubali kumzuia Profesa Lipumba na hata
alipokwenda Sultan wa Pili wa Zanzibar, Jeshi hilo pia lilimzuia kwa
kigezo kile kile kilichomo ndani ya barua ya Barwan.
Alisema hoja kuhusu ushirikiano wa Profesa Lipumba na vyombo vya Dola,
nayo ni hoja dhaifu isiyo na mashiko, kwa kuwa ni Mwenyekiti wa CUF, ni
kiongozi katika jamii na ni daktari wa uchumi anayetambulika hata nje
ya nchi.
Kuhusu madai ya njama za kumwengua Maalim kwenye nafasi ya Katibu Mkuu,
alisema hakuna mwenye njama hizo bali amejiengua kwa mujibu wa Katiba ya
CUF ya mwaka 1992 Toleo la 2014.
“Ndiyo maana hakutaja ibara wala kifungu cha Katiba kilichokiukwa katika
anachokiita njama za kumwengua. Ibara ya 93 kifungu cha 3 kiko wazi,
kwa hivyo asilete blah blah aoneshe ibara au kifungu kilichokiukwa,
vinginevyo itakuwa hadithi za Mfalme Juha,” alisema.
Aliongeza kuwa walio ofisini Buguruni ndio viongozi na wanaoshinda
wakifanya mikutano hotelini kwa fedha za mafisadi, ndio wahuni na ni
muhimu kwa Maalim kutambua kuwa muda si mrefu ubinafsi wake utamdhuru.