Binti mwenye umri wa miaka 12 amejikuta akipoteza haki yake ya kuwa
mtoto baada ya kubakwa, kupewa ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume.
Ni sawa na kusema mtoto amejifungua mtoto.
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inamuelezea mtoto kuwa ni yule aliye na
umri chini ya miaka 18 na kimaadili gazeti hili linahifadhi jina lake.
Mwananchi ilienda maeneo ya Magomeni jijini Dar es Salaam kumshuhudia
mtoto huyo akiwa amempakata mwanae huku akimbembeleza anyonye kwa kuwa
alikuwa akilia.
Uso wake uligubikwa na machozi wakati wote wa mazungumzo na gazeti, na
unyonge ulizidi pale mtoto wake alipolia. Kilio cha kichanga huyo mwenye
umri wa miezi minne, kilitokana na njaa kwa kuwa maziwa ya mama yake
yalikuwa hayatoki.
Bibi yake, Elizabeth Mahundi alisema mjukuu wake, alijifungua kwa njia
ya kawaida Novemba 28, 2016 katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es
Salaam.
“Ni kweli kwamba mjukuu wangu ni mtoto wa miaka 12, hakuna aliyeamini
kama angeweza kujifungua salama lakini, kwa uwezo wa Mungu, imekuwa.
Inahuzunisha, inaumiza naomba Serikali isikae kimya inisaidie,” alisema
na kuongeza:
“Akili yake haipo sawa japo alikuwa akisoma darasa la nne Shule ya
Msingi Pera, ni mtoto asiyeweza kumhudumia mwanaye. Kila kitu nafanya
mimi, na kibaya zaidi sina uwezo kabisa.”
Mtoto huyo alisimulia kinagaubaga alivyofanyiwa ukatili na mwanaume
(Jina linahifadhiwa), ambaye anadai ni mtoto wa shangazi yake.
Simulizi ya mtoto
Mtoto huyo alisema, ilikuwa mchana wakati anatoka shule alipokutana na
mwanaume huyo ambaye alimvutia kwenye pagale (nyumba mbovu). “Nilikuwa
natoka shuleni nikakutana na..., aliniita nikaitika, akanivutia kwenye
pagale,” alisema. Alisema mwanaume huyo alimtaka avue nguo lakini kwa
sababu hakujua kinachotaka kufanyika, aligoma na kuomba arudi nyumbani.
“Alinikamata akanivua nguo zote na akanifanyia kitu kibaya. Nililia
lakini alisema nisimwambie mtu kwani nikifanya hivyo atanifanyia kitu
kibaya tena,”alisema.
Mtoto huyo alisema kuwa alirudi nyumbani kwa bibi yake mzaa baba,
aliyekuwa akimlea katika kijiji cha Pera, Chalinze, Bagamoyo Mkoa wa
Pwani na hakusema kitu akihofia kuumizwa na mbakaji huyo.
“Niliendelea kukaa nikashangaa kila siku nimeshiba, tumbo kubwa ndio
wakaniweka kikao nikawaambia ni... alinifanyia kitu kibaya. Wakasema
nisiseme kwa mtu,” alisema mtoto huyo na kuangua kilio zaidi.
Mtoto huyo anashindwa kuzungumza kutokana na kilio hicho. Wakati huo
mtoto wake aliyekuwa akibembelezwa na bibi alikuwa amelala na hivyo
kulazwa kitandani, kwenye chumba kimoja wanamoishi.
Alisema anaomba aendelee na masomo yake kwani anaamini anaweza kumaliza shule.
“Naomba msaada wa maziwa ya mtoto hayatoki na naomba nisome,” alisema.
Hali niliyoikuta nyumbani
Mwananchi lilifika nyumbani kwa familia hiyo na kumkuta akimbembeleza
mtoto na ilikuwa kama sinema ya mtoto anayecheza na mdoli wake, akiigiza
kumnyonyesha. Lakini hili lilikuwa ni tukio halisi la binti wa miaka 12
akimnyonyesha mtoto wa miezi minne.
“Nyamaza, nyamaza unyonye” ilikuwa sauti ya mtoto huyo akimbembeleza mwanaye.
Bibi Mahundi alisema, mtoto huyo analia njaa. Hata siku Mwananchi
linafika katika familia hiyo, inaelezwa kuwa walishindia uji na hali
hiyo inasababisha mzazi mtoto akose maziwa.
Hatukuweza kuanza mazungumzo, hivyo ikabidi yatafutwe maziwa kwa ajili ya mtoto.
“Maisha yangu magumu, sina kazi na kama unavyoona. Sina namna inabidi
nijitahidi kumlea mjukuu wangu ambaye hajiwezi. Hawezi hata kumfulia
mwanae nguo, ama kweli dunia ngumu,”aliongea bibi ambaye alibubujikwa na
machozi.
Bibi Mahundi alisema siku hiyo hakukuwa na hata tone la unga.
Afya mtoto huyo imezorota na ngozi yake inaonyesha anakosa lishe bora kutokana na hali ngumu ya maisha inayomkabili bibi yake.
Midomo imebadilika rangi kwa kukosa chakula, ni ukweli usiopingika, anahitaji msaada.
Ilikuwaje
Bibi Mahundi anasema ilikuwa saa sita usiku aliposikia mlango unagongwa.
Alifungua na kukutana na mtoto huyo akiwa analia huku akishindwa
kuongea.
“Nilishangaa kuona mtoto wangu analia, wakaniambia wameniletea mtoto
nimuangalie hali yake, nilichungulia nje na kumkuta akiwa na tumbo
kubwa, jasho linamtoka na amechoka sana. Niliishiwa nguvu kwa kweli,”
alisema.
Aliwaambia waingie ndani ndipo wakamwambia kuwa mtoto aliyekuwa akiishi
Pera, Chalinze kwa bibi yake mzaa baba ameletwa akiwa mjamzito licha ya
umri wa miaka 12, alionao.
“Nilimpokea mjukuu wangu, nikalala naye hadi asubuhi. Kulipokucha mama
yake alienda kijijini alikokuwa anaishi lakini aliambulia
kutukanwa,”alisema na kuongeza:
“Aliambiwa kwanza mtoto si wa kwao kwa sababu kule ni kwa bibi mzaa
baba. Na wakajigamba kwamba hakuna sheria inayoweza kuwafanya chochote,
kwa unyonge alirudi, nikamsihi atulie tumtunze mtoto tukimuombea uzima.”
Siku ya kujifungua
Baada ya wiki mbili tangu mtoto huyo awasili Dar es Salaam, alipata
uchungu. Bibi yake alisema walihangaika kutafuta usafiri hadi
Mwananyamala na baada ya muda mfupi, alijifungua kwa njia ya kawaida.
“Nilimshukuru Mungu, sikuamini kama mtoto wa miaka 12 anaweza kujifungua
kawaida. Alikaa hospitali siku saba, kisha tukaruhusiwa kurudi nyumbani
akiwa na afya njema,”alisema.
Mama yake mdogo, Rose John alisema jambo hilo limeiumiza familia nzima.
“Kila nikimuangalia huyo mtoto naishia kulia, natamani kumsaidia lakini
hata mie zaidi ya kufanya kazi za ndani sina msaada wowote. Hakika
naomba Serikali isikae kimya, huu ni ukatili,”alisema.
Waziri atoa tamko
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa hiyo na jitihada
zinafanywa kumkamata mwanaume aliyehusika kwenye tukio hilo.
“Tutahakikisha kijana aliyempa ujauzito binti huyu anakamatwa na
kufikishwa mbele ya vyombo vya dola,” alisema.
Alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watoto wadogo wa kike
wanadhalilishwa na kupewa ujauzito wakiwa na umri mdogo na hivyo kuacha
masomo.
“Hivi kweli tutafikia Tanzania ya viwanda wakati asilimia 27 ya watoto
wa kike wanabakwa na kupewa mimba hivyo? Hakika mimba za utotoni na
ukatili ni kikwazo,” alisema Ummy. Alisema tayari kikosi kazi kimeanza
kufuatilia suala hilo na kuahidi kuwa Serikali itatoa taarifa zaidi ya
kitakachoendelea.
Wanaharakati wazungumza
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, Lilian Liundi alisema lazima
ukimya uvunjwe ili hatua za kisheria kwa aliyehusika kumdhalisha mtoto
huyo kukamatwa.
“Haijalishi ni binamu, mjomba wala nani anapaswa kukamatwa ili hatua
zichukuliwe. Haya masuala ya ndugu ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo kwa
watoto wengi kubakwa, kupewa mimba na kuzalishwa kwenye umri
mdogo,”alisema.
Mama mzazi azungumza
Mama mzazi wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alisema hana la kuzungumza zaidi ya kuomba msaada kwa ajili ya mwanae.
Kwa atakayeweza kuisaidia chakula anaweza kutuma fedha kwa simu 0787 672117
