Kamanda wa polisi
mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, akizungumza
jambo na waandishi wa habari, ofisini kwake. (picha na Mwamvua Mwinyi)
JESHI la polisi
mkoani Pwani, linamshikilia Amiri Alalae (26)mkazi wa Toptop, wilaya ya
Bagamoyo kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu 30 raia wa nchini
Ethiopia.
Kamanda wa polisi
mkoani humo, Onesmo Lyanga, alisema tukio hilo limetokea april 13 majira
ya saa kumi usiku huko maeneo ya Kilomo kata ya Kilomo tarafa ya
Yombo.
Alieleza kuwa askari
wa jeshi la polisi waliokuwa kwenye doria maeneo mbalimbali ya wilaya ya
Bagamoyo walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu hao wakiwa wameingia
nchini bila kibali.
“Wakiwa wamepakiwa
kwenye gari lenye namba za usajili T. 824 DFG aina ya Town hiace pickup
lililokuwa likiendeshwa na Amiri Alalae “alisema kamanda Lyanga.
Kamanda Lyanga
alisema, wahamiaji waliingia nchini kwa njia ya majini wakitumia
majahazi na kushukia maeneo ya bandari bubu ya Jitu Kuu kutoka nchi
jirani ya Kenya.
Alisema watawakabidhi kwa idara ya uhamiaji ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda huyo alitoa
rai kwa wananchi hasa madereva kuacha tabia ya kusafirisha wahamiaji
haramu kwa lengo la kujiongezea kipato.
Alisema kwa kufanya
hivyo ni kinyume cha sheria na kamwe hawatakuwa na muhali na wale wote
wanaofanya biashara hiyo ndani ya mkoa wa Pwani.
Tags
POLISI