Na Lydia Churi- Mahakama, Arusha
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania
Mheshimiwa Prof.Ibrahim Juma amewaagiza Majaji wote nchini kuzipa
umuhimu wa kipekee wa kuzisikiliza na kuzimaliza kwa haraka kesi zote
zenye mvuto kwa jamii na zenye maslahi kwa Umma ili kuongeza imani ya
wananchi juu ya Mahakama kama chombo cha utoaji wa haki.
Akifungua mafunzo ya Majaji wa
Mahakama ya Rufani pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania alizitaja kesi zinazotakiwa kusikilizwa na
kumalizwa kwa haraka kuwa ni zile zinazohusu dawa za kulevya, ujangili,
ugaidi, Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na mauaji ya
vikongwe kwa imani za kishirikina.
Prof. Juma alizitaja kesi
nyingine zinazotakiwa kupewa umuhimu wa kipekee kutokana na mvuto wake
kwa jamii kuwa ni pamoja na kesi za rushwa kubwa, utakatishaji wa fedha,
matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi, na kesi zinazohusu changamoto
za ukuaji wa demokrasia na uendeshaji wa masuala ya siasa.
Kesi nyingine zilizotajwa na Jaji
Mkuu katika kupewa umuhimu wa kipekee ni zile zinazohusu miradi
mikubwa kama Reli, mashamba makubwa ya uwekezaji, gesi, ujenzi wa
barabara, kesi za mabenki na kesi zinazohusisha kundi kubwa la watu
zinazogusa migogoro ya umiliki wa ardhi na migogoro ya wakulima na
wafugaji.
“Tukichukua hatua za dhati
kuhakikisha kesi hizi zinaisha kwa wakati tutakuwa tumetoa mchango
mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama”,
alisema Kaimu Jaji Mkuu.
Alisema ni Jambo muhimu kwa
Mahakama kuzipa umuhimu wa kipekee kesi hizi hasa katika kipindi hiki
ambacho Serikali inatekeleza mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka
mitano (2016/17-2021) ambao kauli mbiu yake ni “kujenga uchumi wa
viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na Maendeleo ya watu”.
Aidha, Kaimu Jaji Mkuu pia
amewataka Majaji kuangalia namna ya kutoa huduma kwa haraka kwenye
makundi yenye mahitaji maalum kama vile wazee, walemavu na wajane
hususan wakati huu ambapo Mahakama inaelekeza nguvu zaidi katika
kuondosha mlundikano wa mashauri mahakamani.
Aliwakumbusha Majaji hao kupanga
kesi kwa siku kwa kuzingatia masaa kama njia ya kuwaepusha wananchi
wenye kesi mahakamani na adha ya kusubiria kwa muda mrefu kesi zao
kuitwa.
Akizungumzia usikilizwaji wa kesi
Mahakamani, Prof. Juma alisema kwa mwaka 2016, Mahakama kuu ya Tanzania
pamoja na divisheni zake zote ilifanikiwa kumaliza kesi kwa idadi sawa
na zilizosajiliwa. Alisema, jumla ya kesi 276,147 zilisajiliwa na kwamba
kesi 278,226 zilimalizika. Kesi 57,326 zilibaki mahakamani.
Alisema bado kuna changamoto ya
mlundikano wa kesi kwenye Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ambapo
lengo kuu la Mafunzo hayo kwa Majaji ni kujadili namna ya kumaliza
mlundikano wa kesi kwenye Mahakama hizi.
Aliongeza kuwa Mahakama za Mwanzo
pekee ndizo zenye mafanikio makubwa ya kutokuwa na mlundikano wa kesi.
Mpaka kufikia Desemba 2016, Mahakama za Mwanzo zilimaliza kesi zote
zenye umri unaozidi miezi sita mahakamani.
Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaendelea na Mafunzo ya siku tano
mjini Arusha ambapo wanajifunza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wao
wa kazi likiwemo suala la kuondosha mlundikano wa kesi kwenye Mahakama
zote nchini.
Tags
SHERIA