Wakati katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif akisema kuwa Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi anakivuruga chama chao, Kamati ya Bunge ya
Sheria na Katiba imemtaka kuhakikisha anamaliza mgogoro wa chama hicho
kuepusha kutia dosari Muungano.
Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya Bunge kumtambua naibu katibu mkuu
wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya kuwa kaimu katibu wa chama hicho kwa
maelezo kuwa Maalim Seif anashindwa kutekeleza majukumu yake.
Bunge lilifikia uamuzi wa kutambua pande zote zinazopingana kwenye
mgogoro huo baada ya Msajili kumwandikia Profesa Ibrahim Lipumba
kumweleza kuwa amekubali ombi lake la kutaka Sakaya atambuliwe kama
kaimu katibu mkuu, jambo ambalo linaonekana kuzidi kukigawa chama hicho.
Profesa Lipumba aliingia kwenye mgogoro na chama chake baada ya kuandika
barua ya kujivua uenyekiti na kukaa nje kwa takriban mwaka mmoja kabla
ya kurejea nchini na kuandika barua ya kufuta uamuzi wa kujiuzulu
uenyekiti, jambo ambalo mkutano mkuu wa CUF ulilikataa na kuridhia
kujiuzulu kwake.
Mgogoro huo umefanya kuwa na pande mbili; wa kwanza ukikubaliana na
uamuzi wa mkutano mkuu wa kuridhia kujiuzulu kwa Lipumba, na wa pili
ukikubaliana na kujirejesha madarakani kwa msomi huyo.
Upande wa kwanza unaendesha shughuli zake kutoka makao makuu ya CUF
yaliyopo kisiwani Unguja na wa pili ukiwa ofisi kuu zilizopo Buguruni
jijini Dar es Salaam.
Jana, kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilimtaka Jaji Mutungi kuchukua
jitihada za kuumaliza mgogoro wa CUF ili kuepusha athari kubwa
zinazoweza kujitokeza katika Muungano.
Akisoma maoni ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu ya mwaka wa 2016/17 na ile ya 2017/18, mjumbe wa kamati
hiyo, Joseph Mhagama alisema mgogoro huo unaweza kusababisha athari za
Muungano.
“Katika mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, Kamati inashauri Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha
mgogoro huo ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika
Muungano,” alisema.
Mhagama alisema kamati hiyo inaiagiza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na weledi katika kusimamia na
utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa na kuhakikisha kwamba taratibu hizo
zinafuatwa katika utoaji ruzuku kwa vyama vya siasa.
Wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani na madiwani, Msajili alitoa
ruzuku ya zaidi ya Sh300 milioni ambazo zilichukuliwa na upande wa
Profesa Lipumba ambao ulibadilisha majina ya watia saini wa akaunti
iliyokuwa wilayani Temeke.
Oktoba mwaka jana, Bodi ya Wadhamini ya CUF ilifungua kesi Mahakama Kuu
dhidi ya Msajili, Profesa Lipumba na wanachama 12 waliosimamishwa.
Pamoja na mambo mengine, bodi hiyo inataka Msajili.
Katika kesi hiyo, bodi inaiomba mahakama ibatilishe barua ya Msajili ya
Septem,ba 23 mwaka jana iliyotengua uamuzi wa Mkutano Mkuu wa kukubali
kujiuzulu kwa Profesa Lipumba, imzuie Msajili asiendelee kufuatilia
suala la kufutwa kwa uanachama wa Profesa Lipumba na pia azuiwe
kuingilia mambo ya CUF.
Jana akizungumza na gazeti hili kuhusu uamuzi wa Msajili kumtambua rasmi
Sakaya kukaimu nafasi yake, Maalim Seif aalisema Jaji Mutungi ndiye
chanzo cha matatizo ya chama hicho.
Alisema Profesa Lipumba si mwanachama wa CUF na pia si mwenyekiti wao kama anavyotambuliwa na Msajili.
“Tangu mwanzo Msajili aliamua kuchukua upande na kuwa pamoja na Lipumba
na ndiye mshauri wake. Wanashauriana kwa kila hali, lakini bado ukweli
unabaki pale pale kwamba Lipumba si mwanachama kwa mujibu wa katiba ya
CUF,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema hata kama Profesa Lipumba angekuwa ni mwenyekiti, hana uwezo kumuengua katibu mkuu wa CUF.
“Chombo ambacho kina uwezo wa kuwashughulikia na kumsimamisha
mwenyekiti, makamu mwenyekiti au katibu mkuu ni Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa. Halafu kama kuna kesi wanapeleka mkutano mkuu ambao unafanya
maamuzi,” alisema Maalim Seif.
“Hata huyo Magdalena Sakaya mwenyewe naye kasimamishwa uanachama, si
mwanachama. Mutungi ndiye anaendelea kulivuruga suala hili kwa mapenzi
yake kwa Lipumba au sijui anapata instruction (maelekezo), sijui. Lakini
Lipumba si mwenyekiti wetu, si mwanachama wa CUF.”
Alisema uchaguzi wa wabunge wa Eala umeharibika kwa sababu ya Msajili kukubali waliowapendekezwa na Lipumba ambao si wanachama.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne, Maalim Seif alipeleka jina la
mgombea mmoja, wakati upande wa Lipumba ulipeleka majina matatu na ofisi
ya Bunge ikayapokea yote, ikiyaweka majina hayo chini ya CUF “A” na CUF
“B” kwa kuzingatia maelekezo ya Msajili.
Maalim Seif alisema Habib Mnyaa, ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Eala
baada ya jina lake kuwasilishwa na Sakaya, alifukuzwa uanachama na tawi
lake na katiba yao inasema hawezi kurudi uanachama hadi miaka miwili
ipite.
“Yote haya Mutungi ndiyo kayachukua yeye ndiyo anavuruga na anaendelea kuvuruga,” alisema.
Jana, Jaji Mutungi alisema hatazungumzia suala hilo tena na vyombo vya
habari, ma kumtaka Maalim Seif asubiri uamuzi wa mahakama.
“Waandishi wa habari acheni kuendesha debate (mjadala) kuhusu suala hili kwa sababu liko mahakamani,” alisema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi ametoa onyo hilo wakati ameshtakiwa mahakamani lakini ofisi
yake ikimwandikia barua Profesa Lipumba kukubali uteuzi wake wa Sakaya
kuwa kaimu katibu mkuu.
Barua hiyo ya Machi 21 imesainiwa na Sisty Nyahoza wa ofisi ya Msajili
na inamweleza Profesa Lipumba kuwa itampa ushirikiano Sakaya katika
majukumu yake ya kukaimu nafasi ya katibu mkuu.
