
Mbunge wa Temeke Mh. Abdallah Mtolea amefunguka na kudai kuwa aliyekuwa
Mwenyekiti wa CUF Prof . Ibrahim Lipumba ni msomi ambaye amejishushia
heshima kwa kufanya jambo la ajabu la kuagiza vijana wake kuvamia
mkutano wa CUF.
Mh. Mtolea amefunguka hayo alipohojiana na EATV na kudai kuwa Lipumba
amefanya vitu vya ajabu ambavyo jamii iliyokuwa inamuheshimu sasa
itampuudha na yeye atapunguza heshima aliyoitengeneza kwa muda mrefu.
"Mimi Lipumba ni kama kaka yangu kwa jinsi nilivyokuwa namuheshimu,
lakini pia alikuwa kiongozi wangu bado namheshimu ila kwa kitendo
kilichofanyika pale VINA nimeishusha heshima yangu kwake kwa kiasi
kikubwa sana na niseme tu amekuwa mtu wa ajabu sana, elimu yake yotee na
heshima aliyonayo amekuja kuiharibu kwa mambo ya ajabu kama
yaliyofanyika"- Mh. Mtolea alifunguka.
Aidha katika hatua nyingine Mh. Mtolea amekiri kusikitishwa na kitendo
cha jeshi la polisi kuzuia mkutano wake uliopangwa kufanyika jana
kujadili jinsi ya kuzitatua kero za wananchi na kuhusisha mkutano wake
na masuala ya kisiasa kitu ambacho kinaweza kurudisha maendeleo nyuma.
" Ni kweli nilipanga kufanya mkutano na wadau wa maendeleo kujadili
changamoto za wananchi wa Temeke haswa wale wanaoishi Kilakala ambao
eneo lote limejaa maji, kwenye eneo lile tumelazimika kuweka pump
inayonyonya maji lakini tulikuwa na changamoto kama mafuta na mambo
mengine hivyo nilikuwa nimepanga kukutana na wadau mbalimbali kwenye
ukumbi wa Temeke Executive lakini ghafla nashangaa nakuja kupewa
taarifa nisifanye mkutano wowote kwa vile eti wamesikia nataka kukutana
na vijana wa CUF ya Lipumba niwashawishi"- aliongeza Mh. Mtolea.
Mh. Mtolea ameendelea kusikitika kwa kudai kuwa kuzuia vikao kufanyika ni kuwanyima wananchi kutimiziwa haki zao za msingi.
"Mimi huwa ni mstaarabu nikitaka kufanya mkutano huwa nawajulisha jeshi
la polisi na wao mara nyingi wamekuwa wakinipatia ulinzi tunashirikiana
vizuri lakini hili la leo nilivyoenda kuwataarifu ni kama nimeenda
kuwambia nizuieni. Hichi kitendo cha kutubana upinzani naona ndicho
kinachoendelezwa zaidi, walitunyima mikutano ya hadhara wakaruhusu
mikutano ya kujadili maendeleo na mimi siku zote huwa nafanya hivyo sasa
nashangaa wamekuja na hii ya kuzuia vikao vya ndani bila kuuliza kikao
kinahusu nini na wakati vinaruhusiwa. Hata kama ni kweli nilikuwa
nakutana na watu wa CUF mimi ni Mbunge katiba ya chama inaniruhusu
kufanya mkutano kwa sababu tayari kwenye chama nina uongozi"- alimaliza
Mh. Mtolea.