WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza
mamlaka za serikali za mitaa, wizara na taasisi zote zitoe taarifa za ajira
zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila robo mwaka.
Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumatano, Aprili 12, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akitoa maelezo ya
kuhitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na
Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Msemaji wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe ambaye aliitaka
Serikali itoe maagizo kwa Wakurugenzi wote wa
Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi
mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa
agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.
“Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, Ibara ya 59 inazielekeza
Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira
katika mipango ya maendeleo ya ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo
wa ajira kila robo mwaka,” amesema.
Waziri Mkuu amesema maelekezo hayo,
yanazingatiwa katika Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali unaotolewa na
HAZINA kila mwaka ambao unazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na
Taasisi zote zibainishe fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka
kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Vilevile mwongozo huo unazitaka taasisi
hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi
hiyo kila robo mwaka. Ninatoa agizo, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na
Taasisi zote ziendelee kuzingatia maelekezo haya,” amesema.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu
amesema ndani
ya mwaka mmoja, jumla ya viwanda 2,169 vimesajiliwa vikiwemo viwanda vya
mbolea, saruji, chuma na vya usindikaji wa mazao.
“Serikali pia inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na
kuvutia uwekezaji nchini. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na
tayari tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, mkoa wa Pwani peke yake una viwanda vikubwa
83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya
Awamu ya Tano,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Mhe.
Jenista Mhagama alisema Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na
Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) ilipanga kukarabati barabara zenye jumla ya
kilomita 148.5, kujenga masoko manne na kukarabati kituo kimoja cha mafunzo ya
utunzaji mazao baada ya kuvuna.
Akijibu
hoja za utekelezaji wa programu hiyo kwa upande wa Pemba na Unguja, Waziri
Mhagama alisema miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ilianza Agosti na
Novemba 2014 na kazi hiyo kwa Pemba ilikamilika Desemba 2015 wakati kwa upande wa Unguja ilikamilika
Januari 2016.
“Kazi
za ujenzi wa masoko
ya Kinyasini na Mombasa
(Unguja) pamoja na Konde na Tibirinzi (Pemba) zilianza Desemba 2016 na zinatarajiwa kukamilika Julai 2017. Wakandarasi
wamehimizwa kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo katika muda uliopangwa ili
kuendana na ratiba iliyopangwa,” alisema.
Akijibu hoja kuhusu uamuzi wa
Serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mhagama alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma na
kuifanya Makao Makuu ya Serikali ilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ambaye alitaka kuona Dodoma ikistawi na Serikali
kuweza kuhamia huko ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya Mji Mkuu.
Alisema
uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma siyo suala la kisiasa kama baadhi ya watu
wanavyodai bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili kama yalivyoelekezwa kwenye
Ibara ya 151 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 na kama ilivyotamkwa
kwenye GN namba 273 ambayo ni tamko la Serikali na sheria halali.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na
Vijana, Mhe. Anthony Mavunde alisema kila mwaka vijana kati ya 800,000 hadi
milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira wakati soko la ajira ni dogo.
Hata
hivyo, Naibu Waziri Mavunde alisema Serikali imeanza kubadilisha mtazamo wa
vijana kuhusu ajira kwani wengi wao hudhani kwamba kuwa na ajira ni lazima mtu
avae tai, awe na ofisi yenye meza na kiti kinachozunguka.
(mwisho)
ma
Tags
WAZIRI MKUU MAJALIWA