
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B,
Assembles of God, Dk. Getrude Rwakatale, amemshukuru Rais Dk. John
Magufuli kwa kumkumbuka na kumteua katika nafasi ya ubunge wa Viti
Maalumu.
Dk, Rwakatale alitoa shukrani hizo Dar es Salaam jana wakati
alipozungumza katika kanisa hilo wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka.
“Leo (jana) tunasherehekea kumbukumbu ya kufufuka kwa mwokozi wetu Yesu
ambaye alitufia pale msalabani,… Pasaka ya mwaka huu ni yangu, Mungu
ameniona.
“Nina furaha ya mwili na roho kwa sababu Yesu amefufuka na pia Mungu
amenirudisha bungeni, Mungu amejibu maombi yetu, tulifunga siku tatu na
ile ya mwisho akajibu,” alisema Mchungaji Rwakatale.
Alisema ana kila sababu ya kumshukuru Rais Dk. Magufuli kwa sababu wapo
wanawake wengi ambao angeweza kuwachagua na kuwapa nafasi hiyo.
“Nakishukuru pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kunikumbuka, wapo
wanawake wangapi lakini leo mlima wa moto katikati ya maombi, Mungu
ametenda,” alisema.
Dk. Rwakatale alitumia ibada hiyo kuwaomba msamaha watu aliowakosea huku akiwasihi waungane naye kumshukuru Mungu katika maombi.
“Katika Luka 24:1-9 tunasoma habari kuhusu ufufuko wa Yesu, tumezoea
makaburini huwa kuna habari mbaya lakini kwa Yesu ilikuwa tofauti,
ilikuja habari njema.
“Alitangaza msamaha hata alipokuwa msalabani basi naomba mnisamehe nilipokosea maana na mimi ni mwanadamu,” alisema.
Aprili 14, mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupitia kwa
Mkurugenzi wa tume hiyo, Ramadhan Kailima ilitangaza jina la Mchungaji
Rwakatale kuwa mbunge baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupeleka jina
lake.
Tume ilipitia fomu zake na kuridhika kuwa mteule huyo ana sifa za kuwa
mbunge akichukua nafasi ya Sophia Simba ambaye alivuliwa uanachama na
chama chake.
Machi 11, mwaka huu, Sophia Simba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake wa CCM (UWT) alivuliwa uanachama kwa madai ya ukiukwaji wa
maadili ya chama hicho na hivyo kumfanya kukosa sifa ya kuendelea kuwa
mbunge kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Tags
Getrude Rwakatare