
KWA mara nyingine wabunge wamekumbushwa kuwa serikali haijazuia mikutano
ya vyama vya siasa nchini, bali kilichofanyika ni kuwekewa utaratibu,
jambo lililosisitizwa lipo duniani kote.
Msisitizo huo ulitolewa bungeni juzi usiku na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Temeke,
Abdallah Mtolea wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyesimama na kulalamikia
kile alichokiita ni vyama vya siasa kuzuiliwa kufanya mikutano ya
hadhara.
Katika kujibu swali hilo, Mwigulu alisema baadhi ya Watanzania
wameshindwa kumwelewa Rais John Magufuli kwa mwongozo na utaratibu
alioutoa huku Waziri Mwigulu akisisitiza kuwa kamwe Rais hajazuia
mikutano ya kisiasa.
Mwigulu alizidi kufafanua kuwa kilichofanyika ni mikutano ya kisiasa
kuwekewa utaratibu kwa wabunge kufanya kazi na mikutano ya kisiasa
katika majimbo yao. “Ni utaratibu wa kawaida kote duniani na mara nyingi
inapangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hasa yanapokuwepo majukumu na
masuala ya kisiasa…majuzi vyama vyote viliruhusiwa kufanya kampeni
katika uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani.
Nani alizuiwa?” alihoji. Akafafanua, “Kilichopo ni kwamba wachaguliwa
wote mnaruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa katika majimbo yenu, ninyi
ni wanasiasa, hamuwezi kuzuiwa kufanya siasa.
Nimshukuru sana Rais (Magufuli), nadhani kwa uzoefu wake kuwa bungeni na
kuwa katika siasa kwa zaidi ya miaka 20, ameliona hili ndiyo maana
akataka uwepo utaratibu ili watu wafanye kazi katika maeneo
wanayowajibika, kule walikopigiwa kura.”
Ufafanuzi huo umekuja baada ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kudai
Rais Magufuli amezuia kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini hadi
mwaka 2020, utakapofanyika Uchaguzi Mkuu, jambo ambalo sio kweli.
Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku mikutano ya kisiasa isiyo na
tija, akiwataka wabunge kusisitiza wananchi kufanya kazi badala ya kila
kukicha kuburuzwa na wanasiasa katika mikutano na maandamano.
Tags
Mwigulu Nchemba