Wakati Mahakama nchini Kenya imezuia kwa muda madaktari kutoka nje
kwenda nchini humo kupiga kazi, zaidi 470 wameomba kazi hizo kupitia
Wizara ya Afya hapa nchini.
Serikali ya Tanzania imesema mchakato wa kupokea maombi hayo pia utaendelea kwa kuwa haijapokea maelekezo yoyote nchini Kenya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amesema bado wanasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Serikali ya
nchi hiyo.
“Tunasubiri taarifa rasmi kutoka Serikali ya Kenya kwa kuwa wao ndiyo
walioleta maombi kwetu. Kama kuna mabadiliko yoyote, naamini
watatufahamisha rasmi,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya
madaktari 470 wametuma maombi kati ya nafasi 500 zilizotangazwa za
kwenda kufanya kazi nchini humo.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsanchiris Mwamaja amesema: “Tumepokea maombi
mengi ya kutosha, lakini ikitokea mtu akatuma tunayapokea, hivi karibuni
jopo litakaa na kuanza kupitia maombi hayo kabla ya usaili na baadaye
kupanga mipango ya namna gani watafika vituo vyao vya kazi.”
Tags
madaktari
