Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amekitaka chama
hicho kumwajibisha Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kwa kauli yake kuwa
alikitoa chama hicho shimoni.
Nape, ambaye alikuwa akishikilia nafasi ya Polepole kabla ya Uchaguzi
Mkuu, alisema maneno hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari
Machi 23, siku moja baada ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza
la Mawaziri.
Nape aliyetishiwa bastola kabla ya mkutano huo, alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Wamesahau wakati mimi nalala porini, wenyewe walikuwa wanakunywa bia
baa. Nimekuwa mzalendo kwa nchi yangu, nimekuwa muungwana kwa chama
changu na ninaapa kuwa muungwana kwa nchi yangu, hilo hakuna
atakayelibadilisha. Lakini mimi nimekuwa mzalendo kwa CCM ambayo
nimeikuta kwenye shimo inakwenda,” alisema Nape.
Lakini Polepole, ambaye jana alitembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi
Communications Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The
Citizen na Mwanaspoti, alisema kama Nape alitoa kauli hiyo, alikuwa
amekengeuka.
“Amekitoa Chama cha Mapinduzi shimoni? Kwamba, wakati anakitoa chama
shimoni wengine walikuwa wanafanya nini?” alihoji Polepole.
Credit - mwananchi
