
SIASA za Ukanda wa Afrika Mashariki zimechukua sura mpya baada ya Waziri
Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa kutangaza rasmi kumuunga mkono Rais
Uhuru Kenyatta.
Kenyatta aliyeunga ushirika pamoja na William Rutto, anaingia katika
kinyang’anyiro cha kuwania awamu ya pili ya kuiongoza Kenya huku upande
wa upinzani ukiwa umepitisha jina la Raila Odinga kupeperusha bendera ya
upinzani.
Wakati Lowassa akitangaza kumuunga mkono Kenyatta, kwa upande wake
Odinga tayari ilishajulikana wazi urafiki wake na Rais Dk. John Magufuli
ambao umeanza miaka mingi tangu akiwa Waziri wa Ujenzi.
Hatua hiyo ya Lowassa ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi
nchini na Afrika Mashariki imekuja baada ya kutembelewa jana nyumbani
kwake Monduli na wabunge zaidi ya 20 na maofisa kutoka Kaunti ya Kajiado
nchini Kenya.
"Mimi naamini Uhuru Kenyatta anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha vema
wananchi wa Kenya na Watanzania. Naahidi ukifika muda muafaka
tutaungana naye kumsaidia katika kampeni zake, alisema Lowassa na
kuongeza:
“Pamoja na kumtumikia Mungu lakini pia kwa moyo wa dhati, mimi na
wananchi wa Monduli tunamuunga mkono Kenyatta katika mbio za uchaguzi
nchini Kenya".
Alisema ushawishi wake kwa Kenyatta umejengwa na imani kubwa aliyonayo
kwa Rais huyo akiamini kwa dhati kwamba ana uwezo mkubwa wa
kuwaunganisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa Tanzania
na Kenya.
"Natamka wazi na dunia yote ijue kuanzia sasa kwamba sisi tunampenda
Uhuru Kenyatta na yeye anajua kama tunampenda, kwa hiyo tunamuunga mkono
tukiamini kabisa ana uwezo wa kuunganisha wananchi wetu,” alisema
Lowassa.
Katika tamko lake, Lowassa mwanasiasa mwenye ushawishi nchini Kenya pia
kupitia jamii ya Kimaasai aliwasihi wananchi wa Kenya kutokufanya makosa
katika uchaguzi ujao.
“Niwaombe wananchi wa Kenya kuhakikisha Rais Kenyatta anarejea madarakani tena kwenye uchaguzi ujao,” alisema Lowassa.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo mzito uliofika nyumbani kwake na
kushiriki pamoja chakula, Naibu Spika wa Kaunti ya Kajiado Dk.Lanoi
Parmuat alimtaka Lowassa katika siasa zake ahakikishe anawashika mkono
zaidi wanawake.
Alisema kina mama katika jamii ndiyo wenye moyo na msimamo thabiti wa kuhakikisha wanamfikisha kwenye ndoto zake za siasa.
“Kwa sasa tunaendesha harakati za kuhakikisha kina mama wa ukanda huu wa
Afrika Mashariki wanakombolewa katika elimu,” alisema Lanoi na
kuongeza:
“Na kwa kupitia hatua hiyo tayari tumewatembelea marais wa Uganda,
Ethiopia na Rwanda na leo tumefika kwako ujumbe wetu mkubwa ukiwa ni
ukombozi wa elimu kwa mtoto wa kike.
“Pamoja na ujumbe huu kufika kwako kukusalimia tunapenda pia
kukuhakikishia kwamba tunaendelea kukuombea kwa Mungu katika uchaguzi
ujao wa Tanzania 2020 uweze kuibuka na ushindi hayo ni maombi yetu kwa
Mungu”.
Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga aliushukuru ujumbe huo kwa kuonyesha
upendo kwa wanananchi wa Monduli na Watanzania kwa heshima
waliyoionyesha ya kumtembelea Lowassa nyumbani kwake na kumtia moyo.
Uchaguzi wa Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu huku kukiwa na
mchuano mkali kutoka kwa wagombea urais kutoka vyama mbalimbali.