| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York, Marekani na kupitisha Azimio la kuongeza muda kwa vikosi vya usalama vilivyopo DRC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy. |
![]() |
| Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Mahiga (hayupo pichani). |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amelipongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kwa kuridhia na kupitisha azimio namba 2348 (2017) la
kuongeza muda kwa Misheni ya Ulinzi wa Amani chini ya MONUSCO iliyopo
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi tarehe 31 Machi, 2018.
Mhe.
Mahiga ametoa pongezi hizo wakati akihutubia Baraza hilo kwenye Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani hivi karibuni.
Mhe. Mahiga ambaye aliwakilisha nchi 15 za SADC alisema kuwa anaupongeza
Umoja wa Mataifa kwa ujumla chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Bw.
Antonio Guterres kwa kufikia uamuzi wa kuongeza muda kwa MONUSCO na
jitihada nyingine nyingi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto
mbalimbali zinazoikabili DRC kwa muda mrefu ikiwemo ukosefu wa amani na usalama.
Mhe.
Mahiga alisema kuwa, kupitishwa kwa azimio hilo kunatoa matumaini mapya
kwa wananchi wa DRC na dunia kwa ujumla kwamba Umoja wa Mataifa una nia
ya dhati kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.
Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kuuomba Umoja wa Mataifa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Kikosi Maalum cha Force Brigade Intervention-FIB kilichoundwa na SADC ambacho kinashirikiana na MONUSCO katika ulinzi wa amani nchini DRC.
Alieleza
kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa FIB kimeonesha
uwezo mkubwa kwa kufanya operesheni ngumu za kukabiliana na vikundi vya
waasi na kuvidhibiti, hali iliyopelekea MONUSCO kuaminika zaidi. FIB
ina mchango wa vikosi vya ulinzi wa amani kutoka nchi tatu za SADC
ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.
“Kuanzishwa
kwa FIB miaka minne iliyopita ulikuwa ni uamuzi wa pekee kwa Baraza la
Usalama na SADC katika masuala ya ulinzi wa amani hususan kwenye maeneo
yenye changamoto kubwa za usalama na amani. Hivyo naamini pamoja na
kwamba FIB ni Chombo cha muda bado kinahitaji kutambuliwa na kupongezwa”
alisema Waziri Mahiga.
Kuhusu changamoto mbalimbali ambazo
MONUSCO inakabiliana nazo ikiwemo matishio mapya ya usalama katika
maeneo ya Kivu, mbinu mpya za mashambulizi za waasi, ukatili kwa raia na
ukiukwaji wa haki za binadamu Waziri Mahiga alisema masuala haya
yanailazimu pia MONUSCO kubadilisha mbinu za operesheni ikiwemo
kuongezewa vifaa na bajeti ili kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto hizo.
Pia
aliliomba Baraza la Usalama, SADC, Umoja wa Afrika, ICGLR na Nchi
zinazoongea Kifaransa kushirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa
changamoto zinazoikabili DRC kwa sasa.
Vile
vile, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya SADC kuiomba
na kuialika Jumuiya za Kimataifa kuisaidia Tume ya Uchaguzi ya DRC ili
iweze kuandikisha wapiga kura na kuandaa uchaguzi nchi nzima. Pia
aliwaomba wanasiasa wa nchini DRC kukabiliana na vurugu za kisiasa
zinazoendelea nchini humo kwa sasa na kukwamisha utekelezaji wa Mkataba
uliofikiwa mwezi Desemba 2016 chini ya Baraza la Maaskofu (SENCO) la
DRC.
Mhe.
Mahiga aliongeza kusema kuwa SADC itatuma Misheni Maalum ya Mawaziri
nchini DRC katika kipindi cha majuma mawili kuanzia sasa kwa ajili ya
kwenda kuzungumza na kushauriana na wadau mbalimbali wa
masuala ya siasa nchini DRC ili kutafuta suluhu.”Sisi , nchi wanachama
wa SADC hatupo tayari kuona Mkataba wa Desemba unakwama” alisisitiza
Waziri Mahiga.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 03 Aprili, 201
Tags
MAHIGA

