SIMBA hakuna kulala, kwani baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Kagera
Sugar, wakifungwa mabao 2-1, sasa wameshtukia mchezo mchafu uliofanyika
na kusababisha kipigo hicho ambapo vigogo wote kwa umoja wao, wameamua
kuungana na kwenda Mwanza kuweka kambi ya muda.
Kikosi hicho kimeongoza ligi kwa muda mrefu, lakini ghafla wakashtukia
wanaenguliwa na watani zao wa jadi, Yanga, baada ya kupoteza dhidi ya
Kagera Sugar na sasa wanaonekana hawataki utani tena katika michezo yao
miwili iliyobakia ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Mbao FC na Toto Africans.
Baada ya kupoteza mchezo huo, baadhi ya mashabiki na hata viongozi
walianza kutoa lawama kwa baadhi ya wachezaji kwa madai ya kucheza
chini ya kiwango, kitu ambacho kimepelekea viongozi kutaka kuchukua
maamuzi magumu ya kuwasimamisha ambao wanadaiwa kuhujumu.
Baada ya mjadala mrefu, vigogo hao kwa kauli moja wamekubaliana kusahau
yaliyopita na sasa wameamua kujikita michezo yao hiyo miwili, wakianzia
na Mbao FC Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya Simba aliliambia DIMBA Jumatano
kuwa baada ya vigogo wote wa Simba kukutana, walikubaliana kuacha kazi
zao na kwenda Mwanza kwa ajili ya kuzuia hujuma nyingine, lengo likiwa
kurudi na pointi sita zilizobakia Kanda ya Ziwa.
“Unajua timu ikifungwa katika mazingira ambayo hayaeleweki lakini kuwe
na maswali mengi ya kujiuliza, lakini nipende tu kusema kwa umoja wetu
tumeamua kupeleka nguvu kubwa jijini Mwanza kuhakikisha tunashinda
michezo yetu miwili.
“Kitu tulichogundua ni kwamba, bado uwezekano wa kutwaa ubingwa upo, ila
kinachotakiwa ni kuzidi kujenga umoja na mshikamano, kwani michezo
mitano iliyobakia si michache,” alisema.
Pia mjumbe huyo alisema wamekubaliana viongozi kuwahoji wachezaji kama
wana matatizo yoyote katika timu kabla ya mchezo wao ujao, ili kama kuna
matatizo yaweze kufanyiwa kazi mapema.
Timu hiyo ipo Geita, ambako itakaa kwa siku kadhaa kabla ya kwenda
Mwanza kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Mbao Jumatatu katika Uwanja wa
CCM Kirumba.
Credit - Dimba
Tags
SIMBA SC
