Hakuna bosi yeyote serikalini anayelipwa zaidi ya Sh17 milioni baada ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kutekeleza sera zake za kubana
matumizi, lakini yupo kiumbe hai mmoja tu ambaye matumizi yake yalifika
Sh64 milioni kwa mwezi; na kuna sababu za kuhalalisha gharama hizo.
Kiumbe huyo ni mnyama mwitu aina ya faru aliyepewa jina la Fausta, ambaye sasa anatumia Sh20.4 milioni.
Fausta ndiye faru kikongwe kuliko wote nchini, akiwa na umri wa miaka
54, na anahitaji matunzo mazuri ili aendelee kuvuta watalii na
wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia.
Fausta anaishi Hifadhi ya Ngorongoro ambako analindwa kwa saa 24
kumuepusha kushambuliwa na wanyama wengine kama fisi na mbwa mwitu
kutokana na uzee, lakini gharama za ulinzi zitapungua baada ya kupata
makazi salama ndani ya mwitu jengo lake litakapomalizika.
Hiyo ni sehemu tu ya gharama zinazomfanya Fausta kutumia fedha nyingi zaidi ya mfanyakazi mwandamizi wa serikalini.
Kazi ipo kwenye malisho
Imeelezwa kuwa sababu zinazofanya matunzo ya Faru Fausta kutumia jumla
ya Sh768 milioni kila mwaka ni pamoja na ulinzi, chakula chake kuagizwa
kutoka nje na miwa anayotakiwa kula.
Sakata la Faru huyo kutumia kiasi hicho cha fedha liliibuliwa juzi na
Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul alipoelezea gharama
hizo na Serikali kuthibitisha.
Hata hivyo, Serikali imesema gharama hizo ni za kawaida kulingana na
thamani na umuhimu wa mnyama huyo ambaye jamii yake iko hatarini
kutoweka.
Meneja wa maendeleo ya tafiti na Ikolojia wa Hifadhi ya Ngorongoro,
Asantaeli Merita alisema jana kuwa matunzo yake yalianza kugharimu fedha
nyingi baada ya kuanza kutunzwa katika eneo maalumu.
Alisema katika eneo hilo ilibidi kujengwa banda lake la kuishi na uzio
wa chuma ambao si rahisi faru huyo kuvunja na kutoka nje. Banda hilo
limezungushiwa mbao maalumu.
Merita alisema kutokana na faru huyo kuwa katika eneo hilo, kuna askari
15 maalumu ambao wanamlinda kwa zamu kwa saa 24 na kuna gari ambalo ni
la mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubeba majani ya lishe kila
siku.
Alisema ili kudhibiti maradhi ambayo faru huyo amekuwa akiugua, Hifadhi
ya Ngorongoro imekuwa ikigharamia chakula cha virutubisho aina ya luseni
ambacho kinapatikana nchini Kenya na amekuwa akipelekewa chakula hicho
mara mbili kwa mwezi.
Alisema luseni anayotumia Fausta ni tofauti na luseni ya ng’ombe wa maziwa ambayo inapatikana hapa nchini.
Alisema faru huyo ‘kikongwe’ pia amekuwa akipewa miwa ambayo inapatikana
eneo la Dareda mkoani Manyara. Miwa hiyo humsaidia kuboresha afya yake
na imekuwa ikipelekwa mara mbili kwa mwezi.
Merita alisema kuna dawa zake ambazo anapaswa kuzitumia kila baada ya wiki mbili.
“Hiyo gharama ya milioni 64 ni ya mwanzo tu baada ya kuanza kuhifadhiwa,
lakini baada ya kupatikana eneo la kumuhifadhi na kujengwa itapungua
sana,” alisema.
Alisema baada ya kukamilika ujenzi wa banda maalumu la kumuhifadhi kwa
sasa wastani wa gharama kwa mwezi zitakuwa Sh20.8 milioni.
Merita alisema kwa maendeleo ya hifadhi ni muhimu kwa Fausta kuendelea
kupatiwa matunzo maalumu kwa kuwa licha ya kuingiza fedha nyingi za
kigeni, pia amekuwa akitumika katika tafiti za wataalumu wa hifadhi za
asili.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikiingiza zaidi ya Sh70 bilioni
kwa mwaka kutokana na watalii ambao wanafika kutembelea eneo hilo.
Karibu nusu ya watalii wanaokuja nchini, hutembelea Hifadhi ya
Ngorongoro.
Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Gekuji alihoji mpango wa
Serikali kwa faru huyo kutokana na gharama kubwa za kumtunza.
“Hifadhi ya Ngorongoro inatumia gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na
kumtunza na kumlisha Faru Fausta. Kiasi cha Sh64 milioni kinatumika kwa
mwezi. Je, Serikali ina mpango gani na huyu Faru Fausta,” alihoji Gekul.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe alisema ni kweli mnyama huyo anatunzwa kwa gharama kubwa kwa
sababu ni mzee na ananyemelewa na magonjwa mbalimbali.
Waziri alisema wanafanya hivyo kutokana na ukweli kuwa wanyama wa aina
hiyo ni wachache katika hifadhi, akasema utafiti unafanyika ili gharama
za kumtunza ziwe ndogo kulingana na thamani inayopatikana. Kiwango hicho
cha fedha kilisababisha Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka
kuomba mwongozo wa Spika.
”Majibu ya waziri anasema Faru Fausta yupo na anatunzwa kwa Sh64 milioni
kwa mwezi. Tafsiri yake ni kwamba anatunzwa kwa Sh768 milioni kwa
mwaka. Anatoa sifa eti kwa sababu ni mzee sana, naomba mwongozo wako
kuhusu hili kwa sababu mnyama huyu hawezi kuingiza faida yoyote,”
alisema Mwakajoka.
Akitoa mwongozo wake Spika Job Ndugai alisema suala hilo anaiachia wizara.
