Hatimaye mvutano wa wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema
umehamia katika ripoti ya utafiti kuhusu masuala ya kielimu uliokuwa
ukitolewa na shirika lisilo la kiserikali la Twaweza.
Wabunge wa Chadema walichangia kwa kueleza namna Serikali ilivyoshindwa
kutambua mchango mkubwa unaotolewa na walimu hasa wa sayansi.
Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha amesema Serikali
imeitelekeza elimu na kuwafanya vijana wa Kitanzania waishi kwa kupata
elimu ya kubahatisha.
Hata hivyo, wabunge wa CCM, Hawa Ghasia na Fatuma Tawfiq ambao walijibu
kuwa kauli za wabunge wa Chadema ni za uchochezi kwa kuwa Serikali
imekuwa ikifanya mambo yake kwa utaratibu na ubora wa hali ya juu.
Awali, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze aliwaambia wabunge kuwa hali
bado ni mbaya kwa wanafunzi wa Kitanzania hasa shule za msingi.
