
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema viongozi
waandamizi wa chama cha wananchi (CUF) ndiyo walihusika na tukio la
kulipua bomu katika nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar baada
ya kufanyika uchaguzi mkuu
Mhe. Masauni alieleza hayo Bungeni Jijini Dodoma jana pindi alipokuwa
akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Gandu kupitia tiketi ya
(CUF) visiwani Pemba, Mhe. Othuman Omary Hajji alipotaka kujua kwanini
mpaka leo hajizachukuliwa hatua stahiki kwa wafuasi wa CCM waliochoma
nyumba za wanachama wa CUF huko visiwani Tumbatu, huku akidai serikali
iliyopo madarakani siyo halali ni haramu kwa kuwa Jeshi la Polisi
lilichangia kumuweka madarakani Dkt. Ali Mohamed Shein.
"Ni kweli baada ya uchaguzi mkuu baadhi ya vyama vya upinzani ikiwemo
chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo
yanayokiuka sheria za nchi yetu.
"Kuna matukio mbalimbali yalijitokeza ikiwemo kuchomwa moto nyumba,
kuchoma mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna wa Jeshi la
Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa, watu
waliokamatwa kwa kuhusika urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni
viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF)". Alisema Masauni
Pamoja na hayo, Masauni alisema Jeshi la Polisi limeshakamilisha
uchunguzi wake na jalada la mashtaka lipo kwa DPP muda wowote kuanzia
sasa litapandishwa Mahakamani ili sheria ichukuliwe.