Kocha Mkuu wa klabu Arsenal
Arsene Wenger amekubali kuchukua mkataba wa miaka miwili katika klabu
hiyo, hatua itakayoendeleza muda ambao amekaa katika klabu hiyo,Mfaransa
huyo amekuwa meneja wa Arsenal kwa miaka 21 sasa.
Wenger na mmiliki wa klabu hiyo
Stan Kroenke walikutana Jumatatu kuamua hatima ya meneja huyo, na kisha
uamuzi wao uliwasilishwa kwenye mkutano wa bodi uliofanyika leo Jumanne.
Arsenal wanapanga kutangaza rasmi uamuzi huo Jumatano.
Gunners walimaliza Ligi ya Premia
wakwia nafasi ya tano, mara yao ya kwanza kumaliza chini ya nafasi ya
nne tangu Wenger alipojiunga nao mwaka 1996.
Walimaliza alama 18 nyuma ya
mabingwa Chelsea, lakini walifanikiwa kuwachapa Blues katika fainali ya
Kombe la FA uwanjani Wembley Jumamosi.
Mkataba wa Wenger ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Wenger aliongoza Gunners kushinda
mataji matatu ya Ligi ya Premia na pia vikombe vinne vya FA misimu yake
tisa ya kwanza kwenye usukani.
Mwaka 2003-04, aliibuka meneja wa kwanza tangu 1888-89 kuongoza timu iliyomaliza ligi kuu bila kushindwa.
Lakini baada ya kushinda Kombe la
FA mwaka 2005, walisubiri kwa miaka mingine tisa – sawa na siku 3,283,
kabla ya kushinda kikombe kingine.
Walilaza Hull City fainali ya Kombe la FA mwaka 2014 na kisha wakashinda kikombe hicho tena mwaka uliofuata.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal
wamekuwa wakimtaka Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 67 ajiuzulu, hasa
baada ya matokeo mabaya msimu huu. Shutuma zaidi zilitolewa
waliposhindwa kwa jumla ya mabao 10-2 na Bayern Munich katika hatua ya
16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Machi.
Walimaliza msimu wakiwa wameshinda
mechi tano mfululizo, lakini matokeo hayo hayakutosha kuwawezesha
kuwapita Liverpool waliomaliza nafasi ya nne na kujaza nafasi ya mwisho
ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Jumamosi, Wenger aliambia BBC
kwamba shutuma na uokosoaji aliokumbana nao msimu huu ni wa
“kufedhehesha” na kwamba hatawahi kuusahau kamwe maishani.
Tags
WENGER