Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (pichani) amewataka maafisa
watendaji wa mitaa,vitongoji,vijiji na kata kuwa chachu ya maendeleo kwa
kushirikiana kikamilifu na madiwani wao ili kuwaletea maendeleo
wananchi huku akiwataka kukataa miradi wasiyoielewa katika maeneo yao.
………………………………………………………………………..
Matiro
ameyazungumza hayo leo May 24,2017 wakati akifunga mafunzo ya siku
mbili ya maafisa watendaji wa mitaa,vitongoji,vijiji,kata na maafisa
tarafa katika manispaa ya Shinyanga yaliyolenga kuwajengea uwezo katika
utendaji wao yaliyofanyika katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna katika
manispaa hiyo.
Matiro
aliwataka maafisa watendaji kuwa makini na miradi inayoanzishwa katika
maeneo yao ili kuepuka kwenye lawama na migogoro inayoepukika na
kukwamisha maendeleo katika jamii.
“Tunahitaji
kuwa na ushirikianona kufanya kazi kwa umoja,nitasikitika sana kuona
mradi unapelekwa kwenye kata yako lakini afisa mtendaji
hauufahamu,ikitokea hivyo ukatae huo mradi kwani inapotokea mradi huo
unaharibika atakayeulizwa ni wewe,kwa hiyo lazima ujue vyema mradi
uliopo katika eneo lako ili kuepuka shida”,alieleza Matiro.
“Nilishawaambia
hata wataalamu wa halmashauri zetu kuwa wanapokwenda kwenye kata au
vijiji wawashirikishe maafisa watendaji kwa wao ndiyo wasimamizi wakuu
wa miradi lakini mnaweza kusimamia miradi hiyo ikiwa mnaitambua na
miradi ambayo hamuitambui ikataeni”,aliongeza Matiro.
Katika
hatua nyingine alisema serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji
watakaoisababishia serikali hasara kupitia fedha mbalimbali zinazotolewa
na serikali kwa ajili ya maendeleo.
Aidha
Matiro aliwasisitiza maafisa watendaji hao kusimamia vyema suala la
ukusanyaji wa mapato na kusimamia vyema suala la ulinzi na usalama
katika maeneo yao.
Matiro
alitumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa watendaji kutatua matatizo ya
wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanatenga siku maalum za kusikiliza kero
za wananchi.
Naye
Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi aliwataka
maafisa watendaji hao kusimamia vyema utaratibu wa kusoma mapato na
matumizi kwa wakati.
Mwangulumbi
pia aliwaagiza maafisa watendaji kutoa ushirikiano kwa maafisa ardhi
wakati wa kupima ardhi,kutunza mali za ofisi na kukusanya mapato katika
maeneo yote ya biashara.
Nao
washiriki wa mafunzo hayo walisema yawasaidia kiutendaji kwani
wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo wajibu wao,umuhimu wa kufuata
taratibu za kazi,kusimamia miradi,uandishi sahihi wa vitabu na nyaraka
za serikali,masuala ya ulinzi,rushwa na tahadhari ya majanga ya moto.
ANGALIA VIDEO HII KUJUA KILICHOJIRI
Tags
WATENDAJI