Imedaiwa kuwa baadhi ya wanasiasa wanaowania nafasi za uongozi katika
Uchaguzi Mkuu ujao Kenya, wameanza kuwasili nchini kusaka nguvu za
waganga wa kienyeji ili washinde katika kinyang’anyiro hicho.
Wanasiasa hao wanaripotiwa kumiminika katika miji ya Tarime, Musoma na
Mwanza ambako hukutana na waganga ili kukamilishiwa mipango ya kushinda
uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.
Taarifa zilizonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya
zinasema waganga hao wamekuwa wakiwapa wanasiasa hirizi ili kuwapoka
wapinzani wao wapigakura.
Gazeti la Taifa Leo limeripoti kuwa, wengi wa wanasiasa hao walianza kumiminika nchini Februari, kabla ya mchujo kufanyika.
“Wengi wa wagombea wanaamini hawawezi kupata ushindi bila usaidizi wa nguvu za kishetani.
Tumekuwa tukiwaona wengi wao wakipitia hapa na kuingia Tanzania,”
alisema mkazi aliyejitambulisha George Ogwang alipozungumza na gazeti la
Taifa Leo.
“Ninamfahamu mmoja wa wanasiasa aliyepokea huduma za waganga hao na bado akabwagwa kwenye mchujo,” alisema.
Kwa miaka mingi wanasiasa katika eneo la Afrika Mashariki wamekuwa
wakihusishwa na waganga wa kienyeji wanapoanza mchakato wa kusaka kura
wakati wa uchaguzi.
Tags
Wabunge