SERIKALI ya Awamu ya Tano imefanya vizuri tangu ilipoingia madarakani,
ikifanikiwa pamoja na mambo mengine kurejesha nidhamu ya kazi na
kuwajibisha viongozi na watumishi wa umma.
Aidha, imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwamo ujenzi
wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ununuzi wa ndege, kuzuia
matumizi yasiyo ya lazima na kufuta maadhimisho ya sherehe mbalilimbali
ni baadhi ya mambo yaliyofurahiwa na wengi.
Hata hivyo, wakati Serikali hiyo inayoongozwa na Rais John Magufuli
ikikaribia kumaliza mwaka wa pili, baadhi ya wasomi na wanasiasa
wametaja mambo 10 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kutokana na utekelezaji
wake kuathiri kundi kubwa la Watanzania wakisema yanaweza kumweka
mtegoni.
Wamesema licha ya kuwa baadhi ya mambo hayo yamefanyika kwa nia njema,
utekelezaji wake ulikuwa na kasoro, huku wakikosoa baadhi ya kauli,
hatua sambamba na kufanyika mambo waliyosema hayana ulazima kwa sasa.
“Matukio hayo yana maana kubwa sana kwani wananchi wamejawa na hasira
hakika wanahifadhi hasira zao kuelekea mwaka 2020,”alisema Zitto Kabwe,
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.
Mambo kumi yanayomweka JPM mtegoni
Mikutano ya hadhara
Marufuku ya mikutano ya siasa mpaka wakati wa kampeni za uchaguzi wa
mwaka 2020 kama ilivyotangazwa na Rais Magufuli ni moja kati ya uamuzi
ulioathiri wanasiasa na vyama, hasa vya upinzani.
Sababu iliyotolewa na Rais Magufuli ni kuwa huu ni muda wa kufanya kazi
na siyo siasa. Katika kufafanua kauli yake, Rais alisema wabunge na
madiwani tu ndiyo wanaoruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo yao na
hawaruhusiwi kuleta wageni kutoka nje.
2. Bomoabomoa
Mwanzoni mwa utawala wake liliibuka zoezi la kuondoa watu waliojenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Bomoabomoa hiyo iliendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuathiriwi
watu wengi masikini ambao ndiyo waliomchagua pia Rais huyo wa Awamu ya
Tano.
Zoezi hilo lililenga nyumba zilizojengwa mabondeni, kwenye fukwe za
bahari ya Hindi, kingo za mito na maeneo ya wazi na hivi karibuni
wamebomolewa waliojenga pembezoni mwa reli ya kati.
3. Matangazo ya Bunge ‘live’
Kusitishwa kwa urushwaji wa matangazo ya Bunge moja kwa moja nao
umewagusa baadhi ya wananchi ambao tangu kutolewa katazo hilo wamekuwa
wakilipinga licha ya kuwa baadhi ya televisheni hurekodi na kurusha
usiku.
Machi mwaka huu chombo kimoja cha habari kiliandika kuwa Rais Magufuli
katika kikao chake cha ndani na wabunge wa CCM mjini Dodoma, aliwaeleza
kuwa yeye ndiye aliyeamua kusitisha mikutano ya Bunge kuoneshwa moja kwa
moja katika televisheni.
4. Wabunge wa CCM kutowatembelea wa upinzani
Katika kikao hicho pia iliripotiwa jinsi Rais Magufuli alivyoshangazwa
na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda
kumtembea mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alipokuwa
gerezani jambo alilolifananisha na usaliti kwa chama chake.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana
na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili. Kauli hiyo ambayo haijakanushwa
popote ilizuia taharuki huku wasomi waliotoa maoni katika gazeti hili
wakitofautiana mtazamo wao.
5. Utumbuaji majipu
Baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka 2015 Rais Magufuli alianza
utekelezaji wa majukumu yake kwa mfumo wa kuwajibisha watendaji wazembe,
wala rushwa na wanaolisababishia Taifa hasara kwa njia mbalimbali.
Mfumo huo wa utendaji kazi umejipatia umaarufu kuwa ‘utumbuaji majipu’.
Licha ya utumbuaji huo kuungwa mkono, wapo walioukosoa wakitaka
watakaotumbuliwa wawe watu waliobainika kuwa na makosa na kasoro
mbalimbali, ukiwakumbe hadi watumishi wasiohusika.
Tangu kuanza kwa utumbuaji, zaidi ya watumishi 1,000 wameshatumbuliwa
jambo linalowafanya katika maisha yao kutosahau utawala wa Serikali ya
Awamu ya Tano.
6. Kufuta safari za nje
Uamuzi wa Rais kubana matumizi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti ziara za
nje zisizo na tija, safari za mafunzo nje ya nchi, warsha, semina,
makongamano na matamasha ulisifiwa na kada mbalimbali nchini lakini kwa
kiasi fulani uliacha simanzi kwa watumishi, hasa waliokuwa wakitumia
maeneo hayo kujipatia fedha za bure.
7. Pesa kutoweka, kupunguzwa kazi
Wapo wanaofurahia hatua za Serikali kuthibiti na kubana matumizi, lakini
uamuzi huo umeathiri sekta nyingi kutokana na fedha kutoweka.
Si hoteli, baa, mashirika ya usafiri, kampuni za huduma za chakula,
vyombo vya habari wala viwanda zilizoepuka athari za uamuzi huo wa
Serikali.
Katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano, ulioshuhudia fedha kutoweka
baadhi ya mashirika na taasisi hasa binafsi zililazimika kupunguza
wafanyakazi wake, huku baadhi ya wafanyabiashara wakifunga biashara
kutokana na mzunguko wa fedha kuwa hafifu wakilazimika kufanya hivyo ili
kwenda sambamba na uzalishaji na kupata faida.
8. Vyeti feki
Uhakiki wa vyeti unaofanywa na Serikali kwa kiasi kikubwa umeacha alama
nyingine kwa Watanzania. Baada ya kupokea majina 9,932 kutoka kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Umma na Utawala Bora), Rais
Magufuli aliagiza wote waliotajwa kughushi vyeti waondoke vituo vya kazi
kabla ya Mei 15 na watakaokaidi watafikishwa mahakamani.
Pengine sio ajabu kutajwa kwenye orodha hiyo kwa kuwa ukaguzi haukuacha
mtu au cheo, lakini kugundulika kwake kunaibua maswali zaidi katika
uhakiki huo ambao tayari uemshaonyesha dosari kama kutaja majina ya
baadhi kuwa wana vyeti vya kughushi vya elimu ya sekondari wakati
hawakuviwasilisha kwenye uhakiki uliofanyika.
9. Tetemeko la ardhi Kagera
Septemba 11 mwaka jana mikoa ya kanda ya ziwa ilikumbwa na tetemeko la
ardhi ambako watu takribani 17 walipoteza maisha, huku zaidi ya nyumba
840 zikibomona na nyingine 1,264 kuharibika.
Wakati akipokea taarifa ya maafa hayo, Rais Magufuli alisema Serikali
itarekebisha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kuwataka
waliobomolewa nyumba, wajipange kuzirekebisha.
Serikali ilizuia watu au taasisi kutoa misaada kwa waathirika, badala
yake ikaagiza wapiti Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku kipaumbele kikiwa ni
kukarabati miundombinu jambo ambalo lilipingwa na kulalamikiwa na watu
waliotaka fedha hizo ziende moja kwa moja kwa waathirika.
10. Kudhibiti mihimili
Licha ya Seriklai kuwa na wajibu wa kutafuta fedha, kitendo cha Mahakama
na Bunge kuwa mihimili inayojitegemea lakini kujikuta ikipangiwa mambo
kadha wa kadha na Serikali kumezungumziwa na wachambuzi wa masuala
mbalimbali nchini kuwa si utaratibu mzuri.
Mfano ni uamuzi wa Rais kuagiza fedha za sherehe ya kuwapongeza wabunge
kutumika kununulia vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Maoni ya wasomi, wanasiasa
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Profesa Abdallah Safari alisema suala la kuzuia mikutano ya hadhara na
kutokuonesha Bunge ni moja ya mambo ambayo yanaweza kumnyima Rais
Magufuli nafasi ya kutetea kiti chake.
“Rais anasema hakuna siasa na wananchi wafanye kazi lakini anashindwa
kuelewa kwamba kuwaminya huko na kuwatengenezea watu hofu ya kushindwa
kuzungumza kunawafanya wazidi kuwa majasiri na siku wakipata nafasi ya
kufanya maamuzi katika chumba cha kura basi hawatomchagua,”alisema.
“Uhusiano wake na wananchi umedorora kwa kuwa anawafanya wawe kimya na
hofu lakini akae akijua kuwa 2020 watu wataikimbia minyororo kwa kuwa
anasema analeta maendeleo lakini utekelezaji hakuna na watu wakijaribu
kumkosoa wanatishwa na kukamatwa.”
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Richard
Mbunda alisema inawezekana Rais akabadilika baadayee kwa kuwa kisiasa
bado miaka ni mingi kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mbunda alisema mbali na mambo hayo, suala la ukata kwa wananchi walio
wengi ndio limegeuka ajenda huku akitolea mfano jinsi anavyozungumzia
hovyo katika mitandao ya kijamii.
“Nadhani demokrasia inawapa nguvu wananchi kuliko viongozi kwa kuwa wao
ndio wanaochagua lakini hapa kwetu viongozi walio wengi huwa
wanyenyekevu pindi wanapoomba kura lakini wakishapata madaraka huwasahau
wapiga kura wao,”alisema.
“Kuna mambo mengi yanaweza kukwamisha safari yake 2020 mfano suala la
kuonekana kutojali wananchi wake ukirejea kauli yake wakati wananchi
wakilalamika njaa, chakula hakuna yeye akawaambia Serikali haitoi
chakula hiyo maana yake Serikali haijali.”
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Onesmo Kyauke alikuwa na mtazamo
tofauti kuwa mambo hayo hayawezi kuwa sababu ya Rais Magufuli kurudi
madarakani lakini akaonya kuwa anapaswa kubadilika ili kurudisha imani
ya wananchi waliyokuwa wamejenga kwake.
“Mfano suala la Bunge Live ni haki ya Wananchi karibu nchi zote duniani
wanonesha Bunge, ni jambo la hatari kuwanyima watu haki zao za msingi,
hata kama Sheria haisemi lioneshwe lakini Sheria hiyo hiyo haikatazi
Bunge Live,”Alisema Dk Kyauke.
Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alitaja uamuzi wa
kufuta mikutako ya hadhara, kubainisha kuwa jambo hilo litampa wakati
mgumu Rais Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.
Tags
RAIS MAGUFULI
