
Malezi ni matendo yote yanayofanywa na wazazi, walezi na jamii kwa lengo
la kumlea, kumkuza, kumlinda, kumuendeleza mtoto kimwili, kiakili,
kijamii, kihisia na kimaadili ili aweze kuishi, kukua vizuri na
kukubalika na jamii.
Ili mtoto aweze kukua katika misingi hiyo muhimu yapo mambo muhimu
ambayo wazazi wanapaswa kuyazingatia wakati wote wa malezi na makuzi.
Mambo hayo ni pamoja na:
Afya
Ili mtoto awe na afya bora, anahitaji kupatiwa kinga zote dhidi ya
maradhi ya kuambukiza kwa njia ya chanjo na kupatiwa tiba mara
anapougua. Magonjwa sugu kama Kisukari, Pumu au Saratani yanaweza
kuathiri makuzi na maendeleo ya mtoto.
Mazingira yanayomzunguka mtoto hayana budi kuwa katika hali ya usafi na
usalama wakati wote. Mazingira hayo ni pamoja na mahali anapolala,
sehemu anazochezea, mavazi na vyombo anavyotumia. Inashauriwa kuwa
wazazi, walezi na jamii wahakikishe watoto wadogo ikiwa ni pamoja na
wale walio katika mazingira magumu zaidi wanapata chanjo kwa wakati na
wanawasaidia kuweka mazingira yao katika hali ya usafi.
Ikiwa mtoto wako ana ugonjwa sugu ni busara kuzungumza na mtaalamu wa
afya ili kuweza kufahamu ni jinsi gani ugonjwa huo utaathiri afya ya
mtoto wako na namna bora ya kumrinda.
Lishe
Ili mtoto aweze kukua vizuri kimwili na kiakili anahitaji chakula bora
au mlo kamili. Chakula bora au mlo kamili unajumuisha vyakula vyenye
virutubisho kama protini, wanga, mafuta, vitamini na madini.
Chakula bora hakina budi kianze kwa mama mjamzito, mara baada ya mtoto
kuzaliwa apatiwe maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya kwanza, baada ya
miezi hiyo mtoto apatiwe vyakula vya kulizika. Mtoto aendelee
kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi miezi 24 na kumpatia vyakula vya
nyongeza.
Ni muhimu mtoto aliye na umri chini ya miaka mitano apate milo
isiyopungua mitano kwa siku na yenye virutubisho vya kutosha.
Inashauriwa virutubisho hivyo vitokane na vyakula vinavyozalishwa katika
maeneo anayoishi mtoto.
Maandalizi ya vyakula vya mtoto yafanyike kwa makini ili visipoteze
viini lishe kwa mfano, ukoboaji wa nafaka mfano mahindi, kuloweka nafaka
na upikaji wa mboga za majani kupita kiasi ni sababu zinazochangia
uharibifu wa viini lishe na ubora halisi wa chakula. Hali hii
husababisha utoaji wa lishe duni kwa mtoto na hivyo kuathiri ukuaji na
uchangamshi kwa mtoto.
Wakati wa kutayarisha chakula, kila kundi la chakula liwepo katika mlo
kamili. Kimsingi, kuna makundi makuu manne ya vyakula. Kundi la kwanza
ni chakula Kikuu mfano nafaka mahindi,
mtama, mizizi (mihogo). Kundi la pili ni vyakula vyenye Utomwili mfano
nyama, samaki, maharage, kunde, mbaazi, Kundi la tatu ni vyakula vyenye
vitamini na madini kwa wingi mfano matunda na mboga za majani na kundi
la nne ni vyakula vyenye nishati kwa wingi mfano mafuta ya kupikia na
sukari.
Uchangamshi
Uchangamshi ni matendo au mwelekeo anaoonyesha mzazi au mlezi kwa mtoto
kwa lengo la kuchochea ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili,
kimaono, kihisia na kimaadili ambapo uchangamshi wa mtoto huanza tangu
akiwa tumboni kwa mama na kuendelezwa baada ya kuzaliwa.
Uchangamshi katika kipindi hiki huchangiwa kwa kiwango kikubwa na hali
ya afya ya mama. Hivyo malezi na uchangamshi wa awali kwa mtoto
unatakiwa uanze mara mimba inapotunga.
Mama mjamzito anahitaji matunzo kimwili, kijamii na kisaikolojia ili
mtoto aliyeko tumboni aweze kukua katika mazingira salama. Ili
kuhakikisha kuwa mtoto anapata malezi changamshi akiwa tumboni wazazi au
walezi hawana budi kuzingatia mambo kama mjamzito kupata mahitaji ya
lazima, asifanye kazi nzito na ngumu, apewe upendo, apate muda wa
kupumzika, mahali pazuri pa kulala,
ahudhurie kliniki pamoja na kupata matibabu na ushauri wa kitaalamu.
Inashauriwa mama mjamzito kutojihusisha na ulevi wa pombe, madawa ya
kulevya, uvutaji wa sigara na vile vile kujiepusha na magonjwa ya
kuambukiza.
Uangalizi
Uangalizi unajumuisha vitendo vitakavyowezesha kuhakikisha kuwa mtoto
yuko katika hali ya usalama ili kulinda uhai na maendeleo ya mtoto.
Vitendo hivyo vinajumuisha kumpatia mtoto mahitaji muhimu kama vile
chakula chenye virutubisho vyote, chanjo dhidi ya magonjwa na tiba mara
anapougua, ulinzi na usalama, kumpakata, kuzungumza naye na kucheza nae.
Hivyo inashauriwa kuwa ni vyema mtoto apewe uangalizi wa kutosha ili
kumwepusha na ajali na mazingira hatarishi yatakayopelekea kuathiri afya
yake, kupata ajali au kufanyiwa vitendo viovu kwa mfano kubakwa.
Ujirani na Jamii inayozunguka
Majirani na jamii inayokuzunguka vina mchango katika malezi na makuzi ya
mtoto wako. Ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto yanachagizwa na
mahusiano mazuri na watoto wenzake, walimu wake na watu wengine
wanaomzunguka.
Lakini vitu kama ufinyu wa makazi, matunzo mabaya ya mtoto au sehemu
isiyo salama kwa mtoto kuchezea au kukaa vinazorotesha ukuaji na
maendeleo ya mtoto.