Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba amefunguka na kusema
jambo alilofanya Rais Magufuli kuzuia mchanga litakwenda kuigwa duniani
kote na kuleta mapinduzi katika "Extractive Industries" (sekta za
uchimbaji madini)
Serukamba alisema hayo jana bungeni na kusema ukiona mpinzani wako
anakupinga katika jambo lolote lile basi ujue umefanya jambo ambalo ni
sahihi ila ukiona mpinzani wako anakusifu ujue umefanya jambo baya,
hivyo kwa kuwa wapinzani wanalalamika basi Rais amepatia katika maamuzi
yake, na anatakiwa kupewa ushirikiano wa wananchi na wabunge.
"Mimi kama mwanasiasa ukiona mtu ambaye ni adui yako umefanya jambo
akakusifia ujue lipo tatizo, ila ukiona umefanya jambo adui yako akasema
umekosea maana yake umepatia sana. Mimi naomba nimpongeze Rais Magufuli
kwa kazi kubwa aliyofanya na niwaambie waheshimiwa wabunge, duniani
kote 'Extractive Industries' inaenda kubadilika atakaye kuwa kwenye
historia ya kubadilisha Extractive Industries ni Rais Magufuli, leo
duniani kote kila kwenye migodi mambo yatabadilika kwa sababu ya
Magufuli amefungua milango, niwaambieni watanzania tusiogope kwenye hili
lazima tuwe nyuma ya Rais tumuunge mkono aendelee na nina hakika
wawekezaji watakuja mezani" alisisitiza Serukamba