Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeahidi kutimiza ahadi
ilizozitoa wakati wa kampeni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na
kusema kuwa muda wa kula matunda ya kazi hiyo umewadia.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo
alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya dhahabu
katika eneo la kitunda wilayani Sikonge mkoani Tabora, amesema kuwa sasa
ni vyema kuhakikisha wachimbaji hao wanatoa ajira kwa wingi kwa wanachi
waliopo katika eneo hilo.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi wakati ikiomba kura kwa
wananchi kuwashika mkono wachimbaji wadogo wadogo na kwa kuwa neema hiyo
sasa imepatikana hapo ni vema vijana wengi wa eneo hilo wenye nia ya
kushiriki katika uchimbaji wa madini wakanufaika na ajira.
“Kila mgodi uwe na majina ya watu wanaotaka kuwaajiri na orodha hiyo
ifike kwa Mkuu wa Mkoa , Maafisa wa Madini wa Kanda ikiwa imeonyesha
jina la kila moja na idadi yao, hatuwezi kuwacha vijana hawa wote bila
ajira,”amesema Muhongo.
Aidha, hatua hiyo imelenga kuondoa tabia ya baadhi ya wachimbaji hao
kuvamia maeneo ya wengine na hivyo kuhatarisha maisha yao naya wengine.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda Kati Magharibi Salim
Salim amesema kuwa ili kuhakikisha maafa mengine hayatokei, kabla ya
kuanza tena uchimbaji katika eneo hilo Ofisi ya Kanda kwa kushirikiana
na Afisa Mkazi wa Madini wameshaanza kusimamia zoezi la kuhakikisha
mashimo ya uchimbaji wa dhahabu yanakuwa kuanzia mita 15 toka moja
kwenda jingine.
Tags
Profesa Muhongo
