
PROFESA wa Uchumi katika Chuo Kikuu Mzumbe, Honest Ngowi, amesema kuna
haja ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha, kuongeza matumizi ya
mashine za kieletroniki (EFD) na kutoa elimu sahihi kwa walipa kodi ili
kuinua mapato.
Pia amesema kuwa mifumo ya usimamizi na utawala wa fedha iimarishwe pia
na utaratibu wa misamaha ya kodi iangaliwe upya kuongeza ufanisi.
Prof. Ngowi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa
wadau wa haki na watetezi wa wananchi kutoka asasi mbalimbali
ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kujadili
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenye
ripoti ya mwaka 2015/16.
Alisema kwenye ripoti ambazo hutolewa mara kwa mara na CAG, pamoja na
mapendekezo na maelekezo kutolewa na Kamati za Kudumu ya Hesabu za
Serikali, hatua zinazochukuliwa bado hazijaleta mabadiliko kwa kiwango
kikubwa.
“Kodi ikikusanywa ipasavyo huduma za jamii kama elimu, afya, miundombinu
zitaboreka na hapa nidhamu katika matumizi ya fedha ni lazima,” alisema
Prof. Ngowi na kuongeza:
“Ripoti inaonyesha kuna matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Mfano kuna
magari 200 yamepewa msamaha kampuni mbili bila utaratibu. Haya ni
matumizi mabaya ya misamaha na hivyo sheria ziangaliwe upya.”
Mkuu wa kitengo cha Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga, alisema
uchelewaji wa fedha za miradi ya maendeleo inasababisha ufujaji wa fedha
na mianya ya rushwa.
Alisema masuala yaliyojitokeza kwenye ripoti ya CAG, ikiwamo kukua kwa
deni la taifa, kuwapo kwa watumishi hewa ambao walilipwa zaidi ya Sh.
trilioni 1.4 pamoja na vyama vya siasa nchini kupata hati isiyoridhisha,
yaangaliwe na kuchukuliwa hatua.