Klabu ya Simba imefanikiwa
kutwaa taji la Azam Sports Federation Cup (FA Cup) baada ya kuifunga
Mbao bao 2-1 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa
Jamhuri, Dodoma kwa dakika 120.
Ushindi wa Simba umewapa ubingwa
wa kombe, pesa kiasi cha shilingi milioni 50 za Tanzania pamoja na
kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la shirikisho barani
Afrika.
Ilikua ni fainali ya aina yake,
soka likapigwa kwa kiwango cha juu na kuburudisha mashabiki walioujaza
uwanja wa Jamhuri kushuhudia fainali iliyozikutanisha timu mbili, moja
ikitoka Magharibi mwa Tanzania huku nyingine maskani yake yakiwa ni
Mashariki.
Dakika 90 zilimalizika timu zote
zikiwa hazijafungana na kulazimika kuongezwa dakika 30 za kuendelea
kumtafuta bingwa mwa mwaka 2017.
Simba walipata bao lao la kwanza
dakika 15 za kwanza za muda wa nyongeza kupitia kwa mshambuliaji wao
raia wa Ivory Coast Fredrick Blagnon.
Mbao walipambana na kusawazisha
bao hilo kipindi cha pili cha dakika za nyongeza na kuwaongezea Simba
mlima ambapo baadhi ya mashabiki walitumaini mchezo ungemalizika kwa
Simba kushinda 1-0.
Kipenzi cha wanamsimbazi Shiza
Kichuya akaipa Simba ndoo kwa kuifungia goli kwa mkwaju wa penati
kufuatia beki wa Mbao kuushika mpira akiwa kwenye eneo la hatari wakati
akifanya harakati za kuokoa.
Penati hiyo ilizua utata baada ya
wachezaji wa Mbao kuanza kumzonga mwamuzi wakipinga maamuzi yake hadi
askari polisi wakalazimika kuwatuliza wachezaji wa Mbao na kuweka
mwamuzi katika hali ya usalama.
Tags
SIMBA NA MBAO