Vijana kutoka mataifa
mbalimbali waliokusanyika katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza
Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN), mjini Arusha wametakiwa
kuchambua masuala yaliyopo mbele yao kwa makini ili kutoa jawabu kwa
matatizo ya dunia yanayohitaji ushiriki wao.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi
wa serikali katika mkutano huo Ngusekela Karen Nyerere, Ofisa
anayeshughulikia dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aliwataka vijana wanaoshiriki
TIMUN kuhakikisha wanaangalia kwa makini mambo yanayogusa nchi zao na
kuyatafutia ufumbuzi kwa kuwa ndio njia pekee ya kutekeleza malengo
endelevu ya dunia ambayo yanahitaji ushirikiano wa ndani na wa
kimataifa.
TIMUN ambayo kirefu chake ni
Tanzania International Model United Nations hufanyika kila mwaka na
ujumbe mbalimbali na mwaka huu ujumbe wa TIMUN ni: “kuwawezesha vijana
katika diplomasia na uongozi”
TIMUN huandaliwa na Shirikisho la
vijana wa Umoja wa Mataifa (YUNA) taasisi ya vijana isiyotengeneza faida
inayotangaza shughuli za Umoja wa Mataifa na kushirikisha vijana katika
utekelezaji wa shughuli hizo.
Aidha aliwashukuru waandazi wa
mkutano huo kubwa unaofanana na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa
(General Assembly) wenye lengo la kukutanisha vijana kujadili
mustakabali wa malengo ya dunia.
Alisema vijana wana nafasi muhimu
katika utekelezaji wa malengo hayo ya maendeleo endelevu jukumu ambalo
dunia imejipa kwa miaka 15 hadi mwaka 2030.
Pamoja na kuwashukuru Taasisi ya
Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) kwa kukubali
kuwa mwenyeji wa kambi hiyo, hali iliyoonesha kwamba wanajali vijana,
mwakilishi huyo wa serikali alisema kwamba Tanzania ipo tayari kusukuma
mbele ajenda ya ushirikishaji vijana katika maendeleo endelevu kwa kuwa
inaamini juu ya hilo.
“Wakati serikali inafanyakazi
kwa karibu na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba malengo ya maendeleo
yanatekelezeka, baraza la vijana ambalo litakutana litakuwa na kazi
kubwa ya kutengeneza sauti ya pamoja namna ya kukabiliana na changamoto
zilizopo”
Alisema kwamba malengo ya dunia
ambayo yapo 17 yanagusa kila sehemu ya maisha na hivyo ni vyema kama
vijana watatoka na majibu ya maswali yanaoumiza vichwa kuhusu malengo
hayo hasa mazingira na dunia endelevu.
Aliwataka vijana kutumia nafasi
yao vyema katika jukwaa hilo kwani maisha ya watu bilioni 7 duniani
wanategemea namna ambavyo wanajengwa na vijana, wenye mchango muhimu wa
kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu.
Awali Mratibu Mkazi wa Mashirika
ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini,
Alvaro Rodriguez alisema kwamba zaidi ya vijana elfu 20 nchini Tanzania
wamefunzwa malengo endelevu ya dunia, toka ulipofanyika uzinduzi Juni,
2016.
Akizungumza katika hafla ya kambi
ya mwaka huu ya Tanzania International Model United Nations (TIMUN),
inayofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela,
Arusha (NM-AIST), Bw. Rodriguez alielezea kufurahishwa na idadi hiyo ya
vijana waliohamasishwa na kusema kwamba malengo ya maendeleo endelevu
2030 yanahitaji kila mmoja kushiriki.
Aidha alielezea umuhimu wa
ushiriki wa vijana katika masuala ya maendeleo kutokana na uwingi wao
hapa nchini. Asilimia 67 ya watu nchini ni vijana.
Bw. Rodriguez alishukuru
machampioni kwa kuwezesha vijana wenzao kutambua malengo endelevu ya
dunia na kuwataka kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwashawishi
vijana wenzao kuelewa na kushiriki katika malengo hayo.
“Nataka kuwatafadhalisha
kwamba huu ni mwanzo tu, kuna mengi ya kufanya. Kama Umoja wa Mataifa,
tunawataka wote mshiriki, si tu katika kuelimisha kuhusu malengo haya ya
dunia, lakini pia katika kuangalia mwenendo wa maendeleo hayo katika
jamii na namna yanavyotekelezwa. Tukio kama hili la TIMUN linasaidia
kuongeza uwezo wa kufikia malengo ya dunia,” alisema Bw. Rodriguez.
Vijana 50 wa kwanza machampioni
walifunzwa mwaka jana katika TIMUN 2016. Kwa sasa kuna vijana
machampioni 500 nchini Tanzania ambao wamepeleka ujumbe kwa vijana
wenzao 20,000.
Ujumbe ambao umekuwa ukisambazwa
na machampioni kwa wenzao umeelezwa kulenga kuchochea hamasa ya kuelewa
malengo kwa ajili ya maendeleo.
“Kama watu hawatajua malengo ya maendeleo endelevu, hawataweza kufanya malengo hayo kuwa ya kweli,”
aliusema ujumbe huo Gloria Nassary, ambaye ni mmoja kati ya vijana 50
waliopewa mafunzo ya kwanza ya kuwa machampioni wa malengo ya dunia.
Naye Tajiel Urioh ambaye ni
Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja
wa Mataifa (TIMUN 2017), pamoja na kusisitiza amani kama sehemu muhimu
ya kusukuma mbele utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu
aliwahimiza vijana kutokata tamaa katika kuhimiza utekelezaji wa malengo
hayo.
Alisema bila amani kuanzia katika
ngazi ya familia, uwezekano wa kutekeleza malengo hayo unakuwa mgumu kwa
kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya amani na utekelezaji wake.
Alisema amani ni kionjo muhimu cha
maendeleo kinapokosekana hata jukumu la vijana kulinda mazingira kwa
ajili ya maendeleo endelevu halitawezekana.
Alisisitiza kulinda mazingira kwa ajili
ya maendeleo na kufikiwa kwa malengo ya Umoja ya Mataifa ambayo ni
malengo ya dunia katika kuimarisha ustawi wa jamii na kuinua uchumi .
Urioh katika mazungumzo yake alisema suala la uchafuzi wa
mazingira ni suala gumu na mtambuka na kwamba mabadiliko ya tabia nchi
yanayosababishwa na kuvurugwa kwa tabaka la ozoni halihusu Ulaya pekee,
ambao wanachafua bali kila mmoja duniani; akiongeza kuwa mwishoni mwa
siku wanaoathirika ni zaidi nchi zinazondelea akitolea mfano nchi za
kusini mwa Jangwa la Sahara.Alisema vijana wanaweza kufanya zaidi ya yale ambayo kwa sasa wameyafanya katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kwamba wana elimu ya kutosha kuhusu malengo hayo na kushirikiana kuyatekeleza kwa kuangalia changamoto mbalimbali ambazo wanazipatia majibu.
Alisema lengo la malengo hayo ni kusaidia jamii vivyo hivyo vijana nao wanatakiwa kujitoa mhanga kuhakikisha kwamba jamii inaendelea kustawi na kuendelea kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Septemba 2015, wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa walikubaliana juu ya malengo mapya ya dunia, malengo ya maendeleo endelevu.
Malengo hayo yanatarajiwa kufanyiwa kazi katika kipindi cha miaka 15 ijayo na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, uchumi na mazingira kwa namna ya kuwa endelevu.
Katika mafunzo hayo machampioni 80 walifunzwa wakiwemo wanachuo 30 kutoka Taasisi ya Uhasibu ya Arusha (Institute of Accountancy Arusha -IAA).
Mkutano huo umefadhiliwa Umoja wa Mataifa (UN), Serikali, Covenant Bank, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) pamoja PIU.
Tags
TIMUN/ DUNIA