Na mwandishi wetu, Zanzibar
Umoja wa Wakulima wa Ndimu wa
Kikundi cha Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini Unguja wametoa kilio
chao cha kukosa soko la ndimu wanazozalisha kwa uongozi wa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Wakizungumza na ugeni huo,
wakulima hao wamesema kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika la
mazao yao kwa kukosa mnunuzi wa uhakika licha ya kulima kisasa na kupata
mazao mengi.
Mmoja wa wakulima hao Bw. Shafi
Hamadi Mussa amesema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika
la mazao ya hali inayorudisha nyuma ari ya kuendelea kulima zao hilo.
“Tunakatishwa tamaa kwa kukosa soko la uhakika licha uwekezaji mkubwa tunaoufanya katika kulima kisasa,” Bw. Mussa alisema.
Bw. Mgana Khatibu Mgana, mkulima
mwengine wa Umoja huo amesema changamoto ya ukosefu wa masoko inaweza
kutatuliwa kwa kupatiwa mkopo nafuu wa kununulia mitambo ya uchakataji
wa mazao ambayo itatumika kuongeza thamani kwa mazao yao.
“Tunauomba uongozi wa Benki ya
Kilimo kutukopesha pesa za kununulia mitambo ya kuchakata mazao yetu ili
kuepuka adha ya ukosefu wa masoko wa mazao haya,’ Bw. Mgana alisema.
Akijibu kilio cha wakulima hao,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema Serikali
imesikia kilio cha wakulima hao kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima
nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo
na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Aliongeza kuwa Benki yake
imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa mazao yote ya wakulima
nchini kwa kuanzia na baadhi ya mazao ili kupata picha halisi ya uhitaji
wa rasilimali fedha kwa wakulima.
“Katika hatua za awali, Benki
imeainisha Minyororo Kumi na Nne (14) ya Ongezeko la Thamani ya Bidhaa
za Kilimo zitakayopewa kipaumbele katika kutoa mikopo ni pamoja na
Kilimo cha Nafaka (Mahindi na Mchele), Kilimo cha Mazao ya Viwandani
(Miwa na Korosho) na Ufugaji wa Ng’ombe (Ng’ombe wa Nyama na Maziwa),”
Bw. Assenga alisema.
Aliongeza kuwa Benki inatoa mikopo
kwa Kilimo cha Mbogamboga (Matunda, Mboga Mboga na Viungo), Kilimo cha
Mbegu za Mafuta ya Kupikia (Alizeti na Ufuta) na kwa upande wa Kilimo
cha Mazao ya Misitu ni Ufugaji wa Nyuki na mazao yake.
Mengine ni Kilimo cha Ufugaji wa Kuku (Kuku wa Kienyeji na wa Kisasa) na Kilimo cha Samaki (Ufugaji wa Samaki).
Bw. Assenga aliwaahidi wakulima hao kuwa TADB itafanyia kazi maombi yao ili kuona namna ya haraka itakayotatua changamoto zao.
Zaidi ya vipaumbele
vilivyoainishwa, TADB pia imejipanga kusaidia minyororo mingine ya
ongezeko la thamani ya mazao ya Kilimo kwa utaratibu maalumu kadiri ya
upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na kusimamia uendeshaji wa fedha
mbalimbali zinazoelekezwa na Serikali ama wafadhili kwenye Sekta ya
Kilimo.
Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) wakikagua mashamba ya midimu wakati
walipotembelea mashamba ya Umoja wa Wakulima wa Ndimu wa Kikundi cha
Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini Unguja.
Hali halisi ya kilimo cha ndimu kijijini Bwejuu, mjini Unguja.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga (kulia) akioneshwa miundombinu ya umwagiliaji ya
kilimo cha ndimu. Anayemuonesha ni Bw. Mgana Khatibu Mgana na (kushoto)
na Bw. Kombo Haji Mussa (katikati).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiangalia namna midimu inavyomwagiliwa maji.
Meneja wa Mikopo wa TADB, Bw.
Samuel Mshote (kushoto) akiangalia ndimu zilizoanguka kwa kukosa wateja.
Kwa mujibu wa wakulima wa ndimu, ndimu huuzwa ikiwa katika hali ya
kijani lakini changamoto za kukosa soko hupelekea ndimu za wakulima wa
Kijiji cha Bwejuu kuivia mtini.
Tags
NDIMU