
Baada ya Shule ya Msingi ya Lucky Vicent kupoteza wanafunzi 32, walimu
wawili na dereva katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu,
wanafunzi wengine wamesema wamebaki nusu ya wanafunzi bwenini.
Kila mwanafunzi ameonekana mwenye hisia katika hafla maalumu ya kuaga
miili ya wenzao kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa na msiba
huu unaonekana utaendelea kuwa katika vichwa vya wanafunzi waliobaki kwa
muda mrefu.
Ndiyo maana imemlazimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Dk Eva Maria Semakafu kutoa ushauri wa uongozi wa elimu
jijini Arusha, kuwatafutia mwalimu wa saikolojia ili awawezeshe
kukabiliana na hali hiyo.
Noreen Josia, mwanafunzi wa shule hiyo anayesoma darasa la sita, anasema hatasahau msiba huo.
Anasema alishtushwa na taarifa kuwa gari lao la shule limepata ajali
kutokana na simu ambazo zilikuwa zinapigwa na pia taarifa kusambaa
kwenye mitandao ya kijamii.
“Nilirudi shuleni kuuliza kama ni kweli, nikaambiwa ni kweli. Tangu
wakati huo hadi sasa, sijisikii vizuri, nahisi kuumwa kwa kuwa bwenini
kwetu karibu nusu ya wanafunzi sijawaona. Nadhani wamefariki,” amesema
huku akitokwa na machozi.
Noreen, ambaye muda mwingi, alikuwa ameshikiliwa na watoa huduma wa
Msalaba Mwekundu, alisema: “Siwezi kusahau kwa kuwa tulikuwa nao bwenini
wakati wakijiandaa kwenda kwenye mitihani ya majaribio Karatu na
tuliagana. Sasa kuambiwa hawapo tena ni jambo ambalo siwezi kusahau,”
anasema.
Noreen anawakilisha idadi kubwa ya wanafunzi wa shule hiyo ambao
wameathiriwa na msiba huo mkubwa wa aina yake na ambao wamepewa siku
saba za mapumziko kwa majili ya kutuliza akili.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ephraim Jackson anasema, wanafunzi 96 wa
darasa la saba ndio walisafiri kati ya wanafunzi 106 wa darasa hilo.