Mkuu wa Wilaya ya Arusha
Gabriel Fabian Daqarro (katikati) akifungua mafunzo ya wajasiriamali
yanayoenda sambamba na utoaji wa mikopo ya wanawake na vijana kwa robo
ya tatu.
Mkurugezi wa Jiji la Arusha
Athumani Kihamia (tatu kulia) akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa
wajasiriamali ambao ni wanufaika wa mikopo ya Halmashauri ya Jiji kwa
robo ya tatu.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel
Fabian Daqarro (katikati) akiwakabidhi hundi ya mfano ya Tsh Mil 390 kwa
vikundi vya wanawake Jiji la Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel
Fabian Daqarro (katikati) akikabidhi hundi ya mfano ya Tsh Mil 336 kwa
vikundi vya vijana, Jiji la Arusha.
Washiriki wakifuatilia mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kukabidhiwa mikopo ya riba nafuu toka Jiji la Arusha
…………………………………….
Nteghenjwa Hosseah – Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.
Gabriel Daqaro amesema wanawake na vijana wanaokidhi vigezo wapewe
Zabuni za Halmashauri ya Jiji ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuboresha
maisha yao kwa kazi mbalimbali zinazotolewa kila mwaka.
Daqaro ameyasema hayo wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya wanawake na vijana ambao ni wajasiriamali
wanaonufaika na mikopo yenye riba nafuu kutoka Jiji ambayo hutolewa kwa
mujibu wa sheria.
“Ni wakati wa wanawake na vijana
kuchangamkia fursa mbalimbali katika Jiji la Arusha ikiwa ni pamoja na
zabuni ambazo zitasaidia kuinua mitaji na kuongeza pato la familia zenu,
hizi kazi ni zenu hakikisheni mnafuata taratibu zote ili mzichukue
wasije watu toka mbali wakapewa wakati ninyi ambao ni wakazi wa Mji huu
mkakosa kwa kukosa vigezo vidogo watumieni wataalamu wa Jiji
wawaelimishe”amesema Daqaro.
Wakati akisema hayo Mkuu wa Wilaya
Mhe. Daqaro amekabidhi hundi za mfano ya Tsh Mil 390 kwa vikundi
vya wanawake 78 huku vikundi vya vijana 67 vimekabidhiwa hundi ya Tsh
Mil 336.
Mhe. Daqaro amesema kuwa kutokana
na changamoto iliyoko katika taasisi za fedha ambazo hutoa mikopo kwa
riba kubwa na kuhitaji dhamana ya nyumba na ardhi jambo ambalo
linawakwamisha wakopaji hivyo Serikali imeamua kutoa mikopo ya masharti
nafuu ambayo ni asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia amewasihi wanufaika wa mikopo
hii kuwa mikopo itumike katika malengo maalumu na katika miradi
inatakayoleta tija kama vile uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo
ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kukuza uchumi.
Kwa upande wao kinamama na vijana
waliopokea mikopo hiyo wamesema kuwa mikopo hiyo itawainua kiuchumi na
kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kuachana na kuwa
tegemezi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na wizi.
Mpaka kufikia robo ya tatu Machi
2017 Halmashauri ya jiji la Arusha imetoa mikopo ya Tsh Bil 1.3 kwa
ajili ya wanawake na vijana kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
Tags
WANAWAKE NA VIJANA