Wasichana 8,000 waliopo
shuleni na 600 ambao hawako shuleni watanufaika na mradi mkubwa wa
kuwawezesha wasichana na wanawake vijana kupata elimu.
Mradi huo wa miaka minne wenye gharama ya dola za Marekani milioni 5 utafanyika katika wilaya tano nchini.
Wilaya hizo ni Ngorongoro, Kasulu, Sengerema, Micheweni na Mkoani.
Mradi huo ambao upo hatua ya pili
umeanza kwa kongamano lililofunguliwa jana na Katibu Mkuu wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo.
Mradi huo mkubwa kwa mujibu wa
Katibu mkuu huyo umelenga kuwaokoa wanafunzi kabla hawajakumbwa na
matatizo yanayokatisha masomo yao.
Aidha utawapa fursa za kuboresha
zaidi mafunzo mbalimbali waliyonayo ambao utawafanya kuwa watu wazuri
zaidi katika jamii na hivyo kuchangia maendeleo ya taifa na jamii
walizopo.
Katibu mkuu huyo ambaye alifungua
kongamano na kuzindua mradi huoi awamu ya pili alisema kwamba ni
matumaini yake kwamba jamii itaukumbatia mradi huo ili kuwa na taifa
lenye mafanikio makubwa katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia
kwa kuzingatia lengo namba tano.
Amewataka wazazi na vijana
kutimiza wajibu wao kwa kubadilika kitabia na kutambua umuhimu wa elimu
katika kufanikisha wanachotaka ambacho ni maendeleo binafsi , familia na
taifa kwa ujumla.
Katika hotuba yake alisema ni
matumaini kwamba wadau katika mradi huo watafaikisha katika kipindi cha
miaka minne mipango yote iliyolenga kuboresha huduma kwa wasichana na
wanawake vijana, kushawishi jamii kubadilika na kuachana na tamaduni
mbaya kama ndoa za utotoni na ukeketaji.
Naye Mwakilishi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na utamaduni UNESCO, Zulmira
Rodrigues alisema mradi huo ulioanza mwaka jana na kufanyiwa tathmini
umeonesha changamoto kubwa ya watoto wa kike ikiwamo mimba za
utotoni,ukeketaji na kushindwa masomo.
Alisema lengo la mradi ni
kuhakikisha kwamba mwanamke anapata fursa za kupambana katika mazingira
yake kama anavyofanya mwanaume kwa kuwezeshwa na kuzuia mila, tabia na
tamaduniu mbaya ambazo zinakwamisha uwezo wake wa kuhudhuria masomo.
Aidha alisema mradi huo utatoa
nafasi kwa wanawake vijana ambao wamekosa masomo au wameacha masomo au
hawakwenda shule kabisa kupata nafasi ya kusoma.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika
la kimataifa la misaada la Korea (KOICA) kupitia UNESCO na kufanyiwa
kazi pia na mashirika ya UN Women na UNFPA unaangalia namna bora ya
kukabiliana na changamoto za mabinti wanaokwenda shule katika wilaya
hizo ili kuwawezesha kuwa watu bora katika jamii siku za usoni.
Mradi huo ni sehemu ya mradi wa
Global Initiative unaoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,
sayansi na Utamaduni (UNESCO), Shirika la Mpango wa watu (UNFPA) na
Shirika la Umoja wa mataifa la wanawake(UN Women) wa kuwawezesha
wanawake kupitia elimu uliozinduliwa katika nchi sita duniani.
Awamu ya kwanza ya mradi huo umelenga kufanywa katika nchi tatu za Mali, Nepal na Tanzania na ulitiwa saini mwaka jana, 2016.
Katika mradi huo serikali ya
Tanzania inawakilishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto; na Wizara ya Katiba na Sheria ambayo ikiratibu mradi kwa niaba
ya serikali ya Tanzania.
Aidha UNESCO inatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na UNFPA na UN Women.
Katika uzinduzi huo Mkurugenzi wa
KOICA Tanzania, Joosung Park pia alizungumza umuhimu wa kufundisha
watoto wa kike na kuwapa fursa na kusema kwamba unapofunza wanawake
unafunza taifa huku akisema kwamba wazazi wanahusika sana katika hilo
akitolea mfano waziri wa mambo ya nje wa Korea wa sasa ambaye ni
mwanamke kwa mara ya kwanza katika miaka mingi ya historia ya nchi hiyo.
Mzungumzaji mwingine ni ambaye
alikuwa Mwakilishi wa UNFPA Tanzania, Dk Hashina Begum alitaka jamii
kuhakikisha kwamba inatoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ili kuzuia
uzazi usiokuwa na mpango ambao unakwamisha maendeleo.
Tags
UNESCO