Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen
Minja akionesha kwa waandishi wa habari vigae vilivyofikishwa katika
maabara hiyo ili kudhibitishwa ubora wake.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen
Minja akionesha kipande cha Bomba kilichohakikiwa ubora katika maabara
hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen
Minja akionesha kwa waandishi wa habari lami iliyofikishwa katika
maabara hiyo ili kudhibitishwa ubora wake kwa mujibu wa sheria ili iweze
kutumika katika ujenzi wa barabara hapa nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen
Minja akipima ubora wa Lami kwa kutumia mashine maalum ili kudhibitisha
kama ina ubora unaotakiwa kulingana na viwango vilivyowekwa.
Mtaalamu wa masuala ya Umeme
kutoka shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. Evance Jeremiah akionesha
namna mitambo ya kupima ubora wa vifaa vya umeme inavyofanya kazi.A
(Picha na Maelezo).
……………………….
Frank Mvungi
MAELEZO
DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka wazalishaji na
wajasiriamali nchini kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha zinakidhi
viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili
kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa Leo Jijini
Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uhandisi wa Ujenzi ya
Shirika la Viwango Nchini, Mhandisi Stephen Minja wakati wa ziara ya
waandishi wa habari kutembelea na kujionea namna maabara za shirika hilo
zinavyotekeleza jukumu lake la kuhakiki viwango vya ubora hapa nchini.
Akifafanua zaidi Minja amesema
kuwa mabara za shirika hilo zipo kwa ajili ya kuhudumia wazalishaji wa
bidhaa mbalimbali na wale wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi lengo
ili kuhakiki ubora wa bidhaa zote ili kuepusha athari zinazoweza
kujitokeza kwa watumiaji.
“Maabara yetu ina viwango vya
kimataifa na gharama zake ni nafuu ambazo kila mwananchi anaweza kumudu
lengo likiwa ni kutoa huduma kwa wananchi na kuchangia kuchochea
maendeleo kwa kudhibiti bidhaa hafifu” alisema Minja
Aliongeza kuwa maabara hiyo
inapima bidhaa za ujenzi kama nondo, chokaa, vigae, mbao, mabomba ya
maji, simenti, nguzo za umeme,matofali,zege, mchanga na bidhaa zote
zinazotumika katika ujenzi wa barabara ikiwemo lami.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa
kitengo cha maabara ya umeme, Mhandisi Anectus Ndunguru amesema kuwa
vifaa vyote vya umeme vinavyozalishwa na kuingizwa nchini lazima vipimwe
ubora wake kuona kama vinakidhi vigezo ili kuepusha majanga.
Alitaja baadhi ya vifaa ambavyo
lazima vihakikiwe ubora wake kuwa ni vifaa vyote vinavyotumika katika
kujenga mfumo wa umeme katika majengo, taa za majumbani, pasi, redio,
televisheni, waya .
Akizungumzia athari za kutumia
vifaa visvyo na ubora Ndunguru amesema kuwa athari za matumizi ya vifaa
hivyo ni makubwa ikiwemo kusababisha majanga na kupotea kwa umeme hivyo
kuongeza gharama kwa mtumiaji.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limekuwa likisisitiza matumizi ya bidhaa zenye ubora na zilizohakikiwa
na kuepuka bidhaa hafifu ambazo kwa sasa zimedhibitiwa na shirika hilo
kwa kiwango kikubwa hali inayochochea ukuaji wa sekta ya Viwanda hapa
nchini.
Tags
BIDHAA TBS