
MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mgwira, ameteuliwa kuwa Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kile kilichoelezwa kuwa ni “mkosoaji mwenye
faida” na kwamba Rais John Magufuli bado ana nafasi kwa wote wanaomkosoa
kwa hoja na si vinginevyo.
Hatua hiyo inatajwa kumweka Magufuli katika taswira ya kukanganya zaidi
kwa kuwa tayari amepata kutoa kauli zinazokandamiza siasa za upinzani
nchini, ikizingatia kuwa Juni, mwaka jana, alitangaza kusitisha mikutano
ya kisiasa akitoa ruksa kwa wabunge pekee hali iliyozua malumbano kati
yake na viongozi wa vyama vya upinzani.
Vile vile akiwa Zanzibar, katika mikutano ya hadhara, mwaka jana,
alimshangaa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kuunda serikali ya
umoja wa kitaifa na wapinzani ambao anaamini hawakustahili kuwamo kwenye
serikali hiyo.
Lakini kwa sasa Raia Mwema limeambiwa na mmoja wa wandani ya Ikulu ya
Magogoni jijini Dar es Salaam kwamba uteuzi huo si wa mwisho na kwamba
Rais Magufuli haamini kwamba kuna watu wameumbwa kuwa wapinzani maisha
yao wote.
Hii ni mara ya kwanza kwa mmoja wa wandani wa Rais Magufuli kueleza
kinagaubaga kuhusu uteuzi huo wa Mghwira ambaye alikuwa mshindani wa
mgombea huyo wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015.
“Nenda kawaambie Watanzania kwamba Mghwira amechaguliwa kwa sababu ya
constructive criticism (ukosoaji wenye hoja) yake. Rais hana shida na
wakosoaji wa namna hiyo na siku zote wana nafasi kwa serikali yake.
“Hata Profesa Kitila Mkumbo naye alikuwa anamkosoa Rais Magufuli mara
kwa mara lakini bado alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Hii ni
kwa sababu siku zote Kitila alikuwa akimkosoa kwa haki na kwa hoja.
“Sasa kuna wakosoaji wengine kila siku wanakosoa tu na wakati mwingine
wanaweka matusi na kashfa humohumo. Watu kama hawa Rais Magufuli hawezi
kufanya nao kazi.
“Na naomba wewe mwenyewe nikupe home work ya kujiuliza nini maana ya
mwanasiasa wa upinzani. Je, maana yake ni kupinga kila kinachofanywa na
serikali iliyo madarakani?
“Kwa tafsiri ya Rais Magufuli, hakuna mpinzani wa kudumu. Yeye anaamini
vyama visivyo madarakani ni vyama mbadala tu kwa CCM na haimaanishi kazi
yao ni kupinga tu bila hoja. Ujumbe kwa wanasiasa wote ni kwamba yeye
hana ubaguzi na yuko tayari kufanya kazi na wote wenye hoja, Raia Mwema
limeambiwa na chanzo chake hicho cha uhakika kutoka Ikulu.
Polepole azungumza
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
alisisitiza kwamba rais amefanya uteuzi huo kwa kuzingatia kigezi kikuu
cha Utanzania wa mteuliwa.
“Ni rais wa Watanzania wote anapofanya uamuzi huzingatia katiba na
sheria za nchi. Amepewa mamlaka kikatiba kuteua wasaidizi wake wakiwamo
wakuu wa mikoa na wilaya, msingi wa kwanza katika uteuzi ni Utanzania wa
watu hao anaowateua na mengine kama uadilifu.
Hizi ni zama za CCM mpya tunatazama uadilifu na kuzingatia watu wenye
fikra na mwelekeo sawa na ule wa rais wetu, kuendeleza mapambano ya
kuelekea uchumi wa kati ambao kimsingi ndio uchumi wa viwanda.
Rais anapofanya uamuzi hafungwi, kuna maeneo anaelekezwa na kuna maeneo
anaachwa afanye kutokana na imani ya wananchi juu yake. Rais anapoteua
Watanzania wanaweza kutoka popote kwenye vyama vya siasa au hata vyombo
vya ulinzi, kuna askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania amewateua kuwa
wakuu wa wilaya kwenye wilaya za pembezoni mwa nchi, hawa bado ni askari
walioko kwenye utumishi wa jeshi,” alisema Polepole.
Credit - Raia Mwema
Tags
anna mghwira