NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NAIBU Spika wa Bunge la Tanzania,
Dk. Tulia Ackson amehimiza watanzania hususan viongozi mbalimbali
kujitokeza kuwezesha matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya
moyo.
Dk. Tulia ametoa rai hiyo leo
alipofanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo
pia alipata fursa ya kumjulia hali mtoto Doreen Sostenes (3) ambaye
matibabu yake yamefadhiliwa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo
anaisimamia.
“Kwa mujibu wa madaktari kuna
zaidi ya watoto 500 ambao wanasubiri huduma ya upasuaji wengi wazazi wao
hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu, Kila mtoto mmoja ni Sh
milioni 2.
“Mimi na Taasisi yangu, tumechagua
kugharamia matibabu ya mtoto Doreen nawasihi wale ambao wanao uwezo wa
kumsaidia hata mtoto mmoja wajitokeze, kwa kufanya hivyo tutazidi
kusaidia wengi, afya zao zitaimarika, wataenda shule, wataelimika na
naamini watakuwa msaada mkubwa kwa Taifa letu baadae,” alisema.
Akieleza kuhusu tatizo
linalomsumbua mtoto huyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto,
Naiz Majani alisema amezaliwa na tatizo la tundu kwenye moyo.
“Moyo una vyumba vinne, viwili
vipo juu na viwili vipo chini, tundu hilo lipo katikati ya vyumba vya
juu na chini, na hivyo kusababisha damu ya safi na chafu kuchanganyika,”
alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ukuaji wa mtoto huyo si mzuri kama ilivyo kwa watoto wa umri wake.
“Lakini magonjwa mengi ya moyo kwa
watoto yanatibika na kupona iwapo wanafikishwa hospitalini kwa wakati
na matibabu huwa ni upasuaji, bahati mbaya wengi wanafika wakiwa
wamechelewa,” alisema.
Tags
magonjwa ya moyo.