MAENDELEO YA TIMU ZA VIJANA.
Ndugu zangu, leo nimewakaribisheni
ili kwa niaba ya Shikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) niweze kutoa
shukrani zetu, pongezi na pia kutoa mwelekeo wa timu zetu za vijana
kuelekea Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 (FIFA WORLD CUP 2026).
SHUKRANI.
Kama tunavyofahamu timu yetu ya
vijana umri chini ya miaka 17 ilishiriki kwa mara ya kwanza katika
Fainali za Afrika (Afcon U17) nchini Gabon, fainali hizi zilichezwa
kuanzia tarehe 14-28 mwezi Mei mwaka huu.
Timu yetu ya Taifa ya vijana umri
chini ya miaka 17 Serengeti Boys ilishiriki katika fainali hizi na
kutolewa hatua ya makundi. Katika hatua hii ilitoa sare ya 0-0 dhidi ya
Mali, ikaifunga Angola bao 2-1 na kutolewa kwa sheria ya uwiano wa
matokeo (head to head) baada ya kufungwa bao moja kwa bila na Niger.
Ni jambo la kutia moyo kuwa bingwa
wa mashindano haya Mali timu pekee ambayo hawakuweza kuifunga ni
Tanzania na timu nyingine zote walizokutana nazo walizifunga ikiwemo na
Ghana ambayo Serengeti Boys walitokana nayo sare hapa Dar es salaam.
Hakika mashindano haya yameonyesha kuwa kumbe Tanzania tunao uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano makubwa.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania linapenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais John
Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu Mh Kassim
Majaliwa ambao kwa umoja wao walihakikisha timu inawezeshwa kikamilifu
na kuwa na nguvu kubwa ya kushindana.
Tunamshukuru sana Mh Dk Harrison
Mwakyembe Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na
watumishi wa Wizara kwa ushirikiano na jitihada kubwa walizozifanya
kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri.
Tunawapa hongera na kuwashukuru
wachezaji wa Serengeti Boys kwa jitihada na ukomavu wao katika kipindi
cha maandalizi na cha fainali zenyewe. Pongezi nyingi na shukrani kwa
benchi la ufundi la timu na uongozi wa timu unaoongozwa na Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF Ndugu Ayoub Nyenzi, Kamati ya Utendaji ya TFF
wakati wote ilikuwa karibu naye na ilimpa nguvu sana. Hongera pia kwa
wafanyakazi wa TFF waliohakikisha wanaratibu shughuli za timu kwa
ufanisi mkubwa.
TFF inawashukuru sana wajumbe wote
wa Kamati ya Uhamasishaji ya Serengeti Boys iliyoongozwa na Bw Charles
Hilary. Uhamishaji wao ulikuwa ni mkubwa sana na uliamsha ari ya
Watanzania kuhamasika na kushangilia timu. Shukrani sana kwa wadau wote
waliochangia timu na shukrani sana kwa waandishi wa habari na wasimamizi
wa blogu mbalimbali na ma admin wa makundi mbalimbali ya mitandao
waliohamasisha na kuichangia timu.
MPANGO WA BAADAYE WA SERENGETI BOYS.
Kikosi hiki cha Serengeti Boys
kilichoshiriki fainali hizi sasa kimebadilika na kuwa rasmi timu ya
Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20 NGORONGORO HEROES. Timu hii mwaka
kesho itashiriki katika hatua hatua za kufuzu kucheza fainali za Afrika
umri chini ya miaka 20 Afcon U20. Fainali hizi zitafanyika mwaka 2019.
Benchi la ufundi la timu hii linaandaa program ya maandalizi ya kikosi
hiki ambayo itahusisha kambi na mechi za majaribio ndani na nje ya nchi.
FAINALI ZA AFRIKA ZA VIJANA UMRI CHINI YA MIAKA 17(AFCON U17) MWAKA 2019.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa
fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tarehe 28
Mei 2017 baada ya mchezo wa fainali za Afcon U17 Rais wa CAF Bw Ahmed
aliikabidhi rasmi Tanzania uenyeji huu kwa njia ya ishara ya kumkabidhi
Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine bendera ya CAF, tukio ambalo
lilishuhudiwa na dunia nzima. Tunamshukuru.
Taratibu za kuandaa fainali hizi
zitaratibiwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya TFF na Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa, na Michezo. Ni Imani ya Shirikisho kuwa Tanzania
itaandaa fainali nzuri na za kihistoria. TFF inatoa rai kwa wadau wote
wa mpira wa miguu Tanzania tushirikiane ili tuzitumie fainali hizi
kujenga jina la nchi yetu kimichezo, kiutamaduni, kiutalii na kiuchumi.
Kwa kuwa Tanzania itakuwa ni
mwenyeji wa mashindano haya moja kwa moja imefaulu kucheza fainali za
mashindano, hivyo Tanzania tutacheza fainali hizi za Afrika mara mbili
mfululizo, jitihada zitafanyika kuhakikisha kombe hili linabakia
nyumbani.
Maandalizi ya timu itakayoshiriki
fainali hizi yalianza mwaka 2015 ambapo TFF iliandaa mashindano ya
kitaifa ya vijana umri chini ya miaka 13 (U13). Katika awamu ya kwanza
ya maandalizi haya Vijana 22 bora waliopatikana kwenye mashindano haya
walikusanywa pamoja na kwa ruhusa ya wazazi wao walipatiwa shule ya
kusoma pamoja ambapo wanapata fursa ya kusoma na kufanya mazoezi ya
pamoja. Shule hii iko mjini Mwanza. Awamu ya pili itakayoanza mwezi
Julai itahusisha vijana hawa kuongeza kasi ya mazoezi na hivyo itabidi
wasome katika shule iliyokaribu na benchi la ufundi la timu hii ambayo
sasa ndiyo rasmi SERENGETI BOYS. Shule hii tayari imekwisha patikana
hapa Dar es salaam na taratibu za masomo yao zinaandaliwa. Tunawashukuru
wazazi wa watoto hawa kwa kutoa ushirikiano kwetu, pia tunaishukuru
shule ambayo wamekuwa wakisomea kwa ushirikiano wao. Mwezi Julai timu
hii itacheza mechi mbili za majaribio za kimataifa. Imani ya TFF ni kuwa
tutajenga kikosi imara cha Serengeti Boys mpya ambacho kitatoa
ushindani na kunyakua kombe la Afcon U17 mwaka 2019.
MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU
(TFF FOOTBALL DEVELOPMENT FUND).
Mfuko huu ulianzishwa mahsusi na
Mkutano Mkuu wa TFF mwaka 2015 kwa ajili ya kukusanya rasilimali za
kuendeshea program za mpira wa vijana na wanawake. Mfuko huu
unajiendesha wenyewe chini ya Bodi yake inayoongozwa na Mwenyekiti Bw.
Tido Mhando. Hivi sasa mfuko huu unaandaa mpango kazi wa miaka kumi
2017-2027 ambao utahakikisha kuwa kuna rasilimali za kutosha za
kuhakikisha:
- 1. Timu zetu za Taifa za vijana Serengeti Boys,Ngorongoro Heroes na Kilimanjaro Warriors zinaandaliwa vyema.
- 2. Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars inaandaliwa na inafuzu kucheza fainali za Afrika za Wanawake mwaka 2018 huko Ghana na hatimae kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2019 huko Ufaransa.
Imani ya Shirikisho ni kuwa
kutokana na jitihada hizi za kujenga vikosi imara vya vijana vya
Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Afrika huko Gabon, Serengeti Boys
itakayoshiriki Fainali za Vijana za Afrika nchini Tanzania mwaka 2019
na Kilimanjaro Warriors (U23) itakayoshiriki hatua ya kufuzu kucheza
Olimpiki Tokyo mwaka 2020 kwa pamoja kuanzia mwaka 2020 kikosi kipya
cha Taifa (Taifa stars) kitaanza kuonyesha uhalisia wa sura yake,
kitalelewa na kitakomaa tayari kushiriki hatua za kufuzu kucheza Fainali
za Kombe la Dunia za mwaka 2026, hatua hizi za kufuzu kucheza hizi
fainali zitaanza mwaka 2024. Shime Watanzania tuunge mkono jitihada
hizi, kwa pamoja inawezekana, fainali za Gabon zimetudhibitishia hivyo!
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki timu zetu zote zaTaifa.
Ahsanteni sana.
Jamal Malinzi
RAIS WA TFF
DAR ES SALAAM
02 Juni 2017.
Tags
MICHEZO