
Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema salfa
iliyoingizwa nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa
matumizi ya kupulizia kwenye mikorosho.
Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati maalum,
waagizaji wa salfa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Korosho nchini (CBT)
kwenye kikao alichokiitisha kwenye makazi yake, Oysterbay, jijini Dar es
Salaam.
“Bodi kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili
waanze kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu
umeshaanza,” amesema.
Juni 4, mwaka huu Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa ulioko bandari ya Dar es
Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI
kuwa ya salfa iliyoingizwa nchini na kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba
ya Bodi ya Korosho haijakidhi viwango.
Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna mkanganyiko
miongoni mwa wakulima juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya kuwa
Serikali ilikwishapokea taarifa ya bodi, na taarifa ya kampuni
iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo
imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa taarifa ya uchunguzi wao mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele
alisema walifanya uchunguzi kwenye makontena 21 ambayo ni sawa na
asilimia 10 ya makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity na moisture
contents kama ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa kutoka GALCO
Inland Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa salfa
ulioletwa na kampuni ya ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema.
“Kwa kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanyika, viwango
(specifications) vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango vya Shirika
la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha salfa ni
maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha (containers) 211
unakidhi viwango,” alisema kwenye taarifa yake.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Maokola Majogo
alisema yeye pamoja na Bodi yake watatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu
na akawataka wakulima wasisite kutumia salfa hiyo kwani
imekwishathibitishwa na Mkemia Mkuu kwamba haina matatizo.
Tags
Majaliwa Kassim