Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro, akifuatilia
taarifa ya utekelezaji ya Mkoa wa Mwanza iliyokuwa ikiwasilishwa na
Katibu Tawala Msaidizi Rasilimaliwatu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Projestus
Rubanzibwa (hayupo pichani) alipokutana na Watendaji wa Sekretarieti ya
mkoa wa Mwanza ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa
Umma 2017.
Sehemu ya Watendaji na Watumishi
wa Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao wakati wa kikao kazi na watumishi hao ikiwa ni sehemu ya
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2017.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisisitiza jambo
kwa Watendaji na watumishi wa Mkoa wa Mwanza wakati wa kikao kazi na
watumishi hao ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
2017.
…………………..
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameelekeza suala
la nidhamu katika Utumishi wa Umma ni namba moja na lipewe uzito
unaostahili ili kujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu.
Dkt. Ndumbaro aliyasema hayo
wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Umma mikoa ya Singida,
Shinyanga na Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi
wa Umma 2017.
Alisema Watumishi wanaokiuka
maadili ya Utumishi wa Umma wasionewe aibu bali wachukuliwe hatua
zinazostahili haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu
na miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.
“Ni lazima hatua za kinidhamu
zichukuliwe mapema kwa mtumishi asiye na maadili kwani bila kufanya
hivyo tutajenga Utumishi wa Umma usio na maadili kwa siku zijazo,” Dkt.
Ndumbaro alisema na kuongeza kuwa mtumishi wa Umma anapofanya kosa ni
lazima lifanyiwe kazi na mwajiri wake katika kituo cha kazi alichopo
badala ya kumhamishia katika kituo kingine.
Aidha, Dkt, Ndumbaro amewataka
waajiri kuwapongeza watumishi wanaofanya vizuri katika utumishi wao ili
kujenga nidhamu ya utendaji kazi.
“Tusifikirie kutoa adhabu tu kwa
Watumishi wa Umma wasio na maadili bali tunatakiwa kutambua mchango na
ubunifu wa wale wanaofanya vizuri kwa kuwapongeza. Tuelewe kuwa
kuwapongeza watumishi wa umma sio lazima tuwape fedha, bali kuwatambua
kwa kuwapa vyeti vya utendaji mzuri na kuwaandikia barua za pongezi kwa
kutambua juhudi zao katika kuwahudumia wateja hivyo kuwapa morali ya
kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na bidii zaidi, aliongeza.
Kwa upande mwingine Dkt. Ndumbaro
amewataka Waajiri kupitia taarifa za Watumishi mara kwa mara ili kuweka
kumbukumbu ya taarifa sahihi na safi katika Mfumo wa Taarifa za
Kiutumishi na Mishahara (HCIMS).
“Waajiri katika Utumishi wa Umma
ni jukumu lenu kuwakumbusha na kushirikiana na Maafisa Utumishi kupitia
taarifa za watumishi mara kwa mara na kuwaondoa katika mfumo wa HCIMS
Watumishi wa Umma ambao hawastahili kuwepo ili kuepukana na suala la
watumishi hewa na taarifa zisizo sahihi (chafu).” Dkt. Ndumbaro
alisisitiza.
Wiki ya Utumishi wa Umma
huadhimishwa kila mwaka na kufikia kilele chake tarehe 23 Juni ambapo
mwaka huu inaadhimishwa kwa viongozi mbalimbali katika Utumishi wa Umma
kukutana ili kufanyia kazi masuala ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu
katika Utumishi wa Umma, pamoja na wadau ili kusikiliza changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika huduma wanazopokea, ndani na nje ya
utumishi wa umma ili kuleta mabadiliko zaidi katika Utoaji huduma na
kufikia malengo ya nchi.