Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Msajili
wa Hazina imeahidi kuendelea kusimamia na kufuatilia sheria na
miongozo yote iliyotolewa ili kuhakikisha lengo la kudhibiti matumizi
yasiyo ya lazima kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ikiwemo safari za
nje na posho za wajumbe wa Bodi za mashirika na Taasisi zote za Umma
linafanikiwa.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa (CCM), Mhe. Japhet
Hasunga ambaye alitaka kujua hatua ambazo Serikali inatarajia kuchukua
kudhibiti matumizi ya fedha za Umma katika Taasisi zake.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali
imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa matumizi ya fedha za Umma
yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu kupitia Sheria mbalimbali
zilizotungwa na Bunge ikiwemo Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015
ambayo imebainishwa hatua mbalimbali za kibajeti zenye lengo la kuongeza
usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma katika Mashirika na
Taasisi za Umma.
“Sheria hiyo imebainisha utolewaji
wa Mwongozo wa Mipango na Bajeti wa Serikali unaojumuisha Mashirika na
Taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbalimbali ya
kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika”, alifafanua Dkt.
Kijaji
Alisema kuwa kupitia Sheria hiyo,
Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia bajeti za
Mashirika na Taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na
mipango ya Serikali inayotarajiwa kutekelezwa.
Mhe. Kijaji alibainisha kuwa
katika Sheria hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu la kupitia
na kuridhia kanuni za fedha za Mashirika na Taasisi zote za Umma ili
kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma.
“Sheria nyingine iliyopitishwa na
Bunge ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 ambayo iliweka
ukomo kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato
yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara”, aliongeza Dkt.
Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema
kuwa katika kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa Hazina inatekeleza majukumu
yake kisheria, imetoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti
matumizi ya Mashirika na Taasisi za Umma ili kupunguza matumizi ya
Serikali yasiyo ya lazima.
“Miongoni mwa miongozo hiyo ni
barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015 ya
kudhibiti safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa watumishi wa
Mashirika na Taasisi za Umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu
kubwa ya fedha za Umma”, alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa waraka wa Msajili
wa Hazina Na. 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi ya
Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma pia ni miongoni mwa miongozo
ya kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwani waraka huo umefuta posho za
vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne
kwa mwaka.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Waraka wa
Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu kwa
Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma ulikuwa
na lengo la kuendeleza jitihada za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima ya fedha za Umma.
Alisema kuwa Waraka huo uliweka
ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje ya
nchi, huku akisisitiza kuwa bado Serikali itaendelea kuhakikisha
matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu