
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kuokoa Sh
bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizofanywa
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mwaka
2016/2017.
Amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno, ikilinganishwa ni Sh
bilioni 7 tu zilizookolewa katika mwaka 2015/2016. Alisema hayo jana
wakati akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge wa Afrika walio katika
Mapambano ya Rushwa (APNAC) Tawi la Tanzania kwenye ukumbi wa African
Dream mjini Dodoma.
Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika
mapambano dhidi ya rushwa, alisema Serikali imeanza kupata mrejesho
mzuri kwamba watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya
rushwa vinaendelea kupungua.
“Baadhi ya hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya
TAKUKURU; kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza
mianya ya kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia
nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu
na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” alisema.
Aliwaomba wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali, kwani haina mzaha
kwenye mapambano hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya
rushwa na tutaendelea na mapambano hayo.
Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika
mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono
kwenye vita hii,” alisisitiza.
“Tayari tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za
ardhi, uchukuzi, biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo.
Tutaendelea kuiwezesha TAKUKURU ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza
ya kubaini mianya na kutoa ushauri wa kuziba mianya hiyo ya rushwa.
Lengo letu ni kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa kuwa kinga ni bora
kuliko tiba”. Mapema, akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angellah Kairuki alisema Takukuru kwa kushirikiana na
taasisi zilizo chini yake, wako njiani kuanzisha mtaala wa somo la
rushwa ili ifundishwe tangu shuleni.
“Napenda kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba Serikali ya awamu ya
tano haitakubali kuona rushwa ikiota mizizi. Tunaamini wanafunzi
wakijengewa uwezo tangu utotoni, watachukia rushwa na hatimaye tutakuwa
na Taifa lenye watu waadilifu,” amesema.
Alisema kutokana na kazi ya kupunguza watumishi hewa, hadi kufikia
Aprili mwaka huu, Serikali imekwishapokea Sh bilioni 1.2 kwenye akaunti
maalumu ya Takukuru iliyoko Hazina ambazo zinatokana na makusanyo kutoka
kwa waliokuwa watumishi hewa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Godfrey Mulisa alisema
wataendelea kushirikiana na Bunge katika miradi mbalimbali ikiwemo
shughuli zinazofanywa na APNAC.
Awali, Mwenyekti wa APNAC tawi la Tanzania, George Mkuchika alisema hadi
sasa wabunge wapatao 148 wamekwishajiunga na mtandao huo. Kwamba
anaamini hadi Bunge hili litakapomaliza muda wake, zaidi ya robo tatu ya
wabunge watakuwa wamejiunga
Tags
RUSHWA