Katibu Mtendaji wa Baraza la
Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mungereza aliyemwakilisha Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe akishiriki kubeba
jeneza lililobeba mwili wa mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha)
anayesadikiwa kuwa mbunifu wa Nembo ya Taifa mara baada ya zoezi la
kuuga mwili huo kumalizika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini
Dar es Salaam leo. Mwili huo umesafirishwa kuelekea Misungwi Mkoani
Mwanza kwa ajili ya mazishi.
………………………………………………………………..
Na: Frank Shija – MAELEZO
Wasanii nchini watakiwa kufuata
taratibu na kujiunga katika vyama vyao ili kujiweka katika mazingira
rafiki ya utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kusaidiana katika kutatua
changamoto zinazowakabili.
Wito huo umetolewa leo na Katibu
Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Godfrey Mungereza ambaye
alimwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe katika zoezi la kuaga mwili wa anayedaiwa kuwa mbunifu wa
Nembo ya Taifa, Mzee Francis Maige Kanyasu zoezi lililofanyka Hospitali
ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam leo.
Mungereza alisema kuwa utaratibu
wa kuwepo kwa vyama vya wasanii ni wa ,uda mrefu tangu miaka ya sitini
ambapo wasanii wamekuwa wakijiunga katika vyama hivyo kwa leong la kuwa
na sauti ya pamoja.
“Mhe. Waziri anasema wazee wa
namna hii,na wasanii kwa ujumla ni vizuri tukafuata taratibu kwa mujibu
wa sheria, hii itasaidia wasanii kutambulika,kujitangaza na
kufahamiana,” alisema Mungereza.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Dharura kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma
Mfinanga alisema kuwa Mzee Ngosha amefariki kutokana na maradhi makubwa
ya Kifua Kikuu kilichotokana na kuugua kwa muda mrefu bila ya kupatiwa
matibabu.
Aidha Dkt. Mfinanga alitumia
fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwahi kufika
katika vituo vya tiba punde wanapohisi kuwa na matatizo ya kiafya kwani
kufanya hivyo watakuwa wamejiweka katika mazingira mazuri ya kuepuka
vifo visivyotarajiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Malapa, Buguruni ameipongeza Serikali kwa jitihada
ilizofanya za kuhakikisha inawapata ndugu zake jambo lililopelekea mzee
Francis Kanyasu kusafirishwa na kwenda kuzikwa nyumbani kwao katika
Kijiji cha Igokero Misungwi Mkoani Mwanza.
Marehemu Mzee Francis Maige
Kanyasu maarufu Ngosha alifikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
mnamo tarehe 25 Mei akitokea katika Hospitali ya Rufaa ya Amana kufuatia
jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto ambapo alifanyiwa vipimo na matibabu hadi mauti
yalipomkuta majira ya saa 2:30 usiku siku ya tarehe 29, Mei, 2017.Mzee
Ngosha anadiawa kuwa miongoni mwa wabunifu wa Nembo ya Taifa jambo
ambalo amekufa kukiwa hakuna uhakika juu ya suala hilo.
Tags
wasanii