Jovina Bujulu,MAELEZO.
Hivi karibuni , Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu ameagiza
Halmashauri zote nchini kuwaadalia na kuwapa wazee vitambulisho vya
kupata huduma za matibabu bila malipo katika hospitali , vituo vya afya
na zahanati za umma katika maeneo yao.
Waziri Ummy amewapa muda hadi
kufikia Desemba 30, mwaka huu wawe wametekeleza agizo hilo. Kwa
kuzingatia na usumbufu ambao wazee wamekuwa wakiupata wanapokwenda
kupata matibabu katika vituo vya afya utekelezaji wa agizo hilo
litakuwa ni mkombozi kwao ili nao wapatiwe matibabu yanayostahili.
“Baadhi ya wazee wamekuwa wakipata
tabu ya kupata huduma bora katika hospitali za umma, natoa wito kwa
wakurugenzi kupunguza kadhia wanayopata wazee hao wanapokwenda kutibiwa ,
hakikisheni mnawapatia vitambulisho wazee wote wasiokuwa na uwezo “
alisema Waziri Ummy.
Vitambulisho hivyo vitawapa fursa
ya kutibiwa bure na hivyo watapata motisha ya kwenda kupata matibabu
katika hospitali mbalimbali bila kutoa malipo yoyote. Kabla ya agizo
hilo wazee kuanzia miaka 60 walikuwa wanalazimika kupata barua kutoka
kwa watendaji wa Serikali za Mtaa ili waweze kutibiwa bure
Utaratibu huu kwa kiasi kikubwa
ulikuwa na usumbufu ambapo walikuwa wanatakiwa kwenda kuchukua barua kwa
Watendaji wa Serikali za Mitaa kila wanapoumwa na barua hizo zilikuwa
zinawawezesha kutibiwa bure kwa wakati huo na endapo wataumwa tena
wanalazimika kufuata barua tena.
Serikali ilifanya uamuzi wa kuwa
na Sera ya Wazee mwaka 1999, katika maadhimisho ya mwaka wa Kimataifa wa
Wazee. Maamuzi hayo yalikuwa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya
kuweka masuala ya wazee katika agenda za maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja na kuwa Serikali
inawatambua wazee kuwa ni rasilimali na hazina kubwa katika maendeleo
ya nchi yetu, wazee hao wanakabiliwa na matatizo ya umaskini,
kutotosheleza kwa huduma za afya, pensheni na kutoshirikishwa katika
maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi yetu. Wazee wengi huishi katika
hali ya umaskini inayoleta mashaka makubwa kwao na takribani asilimia
75 wazee wanaishi vijijini.
Taarifa za Umoja wa Mataifa za
mwaka 1999, zinaonyesha kuwa katika Afrika , Tanzania ni nchi ya pili
kuwa na sera ya wazee baada ya nchi ya Mauritius.
Kupitia Sera hiyo Serikali
iliahidi kuhakikisha kuwa wazee wanatambuliwa na wanapata fursa ya
kushiriki katika maendeleo ya nchi sambamba na wananchi wengine.
Aidha taarifa hizo zinaendelea
kuonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wazee duniani na hasa
katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na
uwezo wa rasilimali zilizopo kuwahudumia katika nyanja za afya, lishe,
na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka
1950, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwepo kwa watu milioni 200 wenye umri
zaidi ya miaka 60, na mwaka 1975, idadi iliongezeka kufikia milioni 350
na ilitegemea kuongezeka kufikia milioni 625, ifikapo mwaka 2005 na
idadi hiyo itazidi idadi ya vijana na watoto wenye umri wa miaka 24
ifikapo mwaka 2050.
Barani Afrika idadi inategemea
kuongezeka kutoka milioni 38 za mwaka 1999, na kufikia milioni 212
ifikapo mwaka 2050. Kwa kuangalia ongezeko hilo la wazee ni wakati
muafaka wa kuwapatia vitambulisho ili kuwapunguzia adha ya kupata huduma
za afya.
Sera ya Taifa ya Afya na Sheria ya
Utumishi wa Umma nchini Tanzania zinazingatia umri wa miaka 60 kuwa
ndio kigezo cha uzee , hivyo kwa sera hii mzee ni mtu mwenye wa miaka
60 na kuendelea. Madhumuni ya sera hii ni pamoja na kuwatambua kama
rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa letu na kuhakikisha kuwa
wazee wanapata huduma zote za msingi zikiwemo huduma za afya.
Nchini Tanzania wazee wapo katika
makundi mbalimbali ambayo ni wazee wastaafu, wakulima, wafugaji wavuvi
na wale wasio na ajira ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa
nguvu za kufanya kazi.
Mazingira ya wazee hao ni pamoja
na matunzo duni, umaskini, magonjwa ya muda mrefu, lishe duni , huduma
za afya kuwa ghali na wao kushindwa kuzimudu, na kuhitaji uangalizi na
matunzo maalum ya kitaalamu.
Kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa
vitambulisho vya matibabu kwa wazee , Serkali imetekeleza ahadi ya
kurekebisha Sera ya kuchangia gharama za afya kwa kurekebisha vigezo
vya utambuzi wa umri wa miaka 60 na kuweka utaratibu wa kufuatilia afya
za wazee katika jamii.
Wazee wote wenye sifa za kuwa na
vitambulisho hivyo ni budi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupatiwa na
kuwaondolea kabisa adha ya kupata huduma za matibabu katika hospitali za
umma.
Tags
Afya ya Wazee