Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi na
wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo waliokuwa
wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.
“Mkurugenzi haya mambo ya
mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa
wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo hili ili waweze kuuza
mazao yao au samaki?”
“Ninakuagiza Mkurugenzi, kesho
Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa Biashara wako, Mwenyekiti wa kijiji na
watu wako pamoja na Diwani wa hapa, itisheni kikao na muonyeshwe eneo la
soko ili mliingize kwenye mipango yenu,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.
Awali, Waziri Mkuu alimwita
Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye Halmashauri yake
kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.
Akitoa majibu mbele ya Waziri
Mkuu, Bw. Mwaiteleke alisema hawajawahi kupata mpango kutoka kwenye kata
hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue mpango huo na kuuwasilisha
kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga fedha za kujenga soko.
Mapema, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kigongo, Bw. Sebastian Kisumo alimweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo
linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na uhaba wa maji.
Kuhusu maji, Waziri Mkuu alisema
Serikali imetenga sh. bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka
Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao utasambaza maji kwenda Misungi,
Usagara hadi Kigongo Feri.
Tags
MAJALIWA