Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe amempongeza Mwenyekiti wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dionis Malinzi kwa hatua kadhaa
ambazo baraza lake limeanza kuchukua katika kusimamia michezo nchini,
likiwemo zuio kwa viongozi kuwa na kofia mbili kwenye mchezo mmoja.
Katika salamu alizomtumia kiongozi huyo wa BMT jana jioni, Dk. Mwakyembe amesema hatua hizo zimeonesha uhai, uhalali na hitaji la uwepo wa BMT kwa maendeleo ya michezo nchini.
Dk. Mwakyembe amesema Wizara haitarajii tena kuona kiongozi
katika mchezo wowote ule nchini kuwa na kofia mbili kinyume na sheria na
kanuni zilizopo, huku BMT ikiangalia pembeni na kuinyamazia hali hiyo.
Waziri Mwakyembe vilevile amesema Wizara haitarajii kuona
chombo chochote cha michezo nchini kikikiuka Kanuni na Sheria za nchi
bila kuchukuliwa hatua stahiki kwa kisingizio kuwa kinawajibika kwa
vyombo vya kimataifa, kwani kisingizio hicho ni batili kikatiba na
kisheria hivyo hakiwazuii BMT kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria
za nchi.
Aidha amewapa pole BMT kwa
kuondokewa na mwanamichezo maarufu nchini Ally Mohammed, a.k.a. Ally
Yanga, aliyefariki dunia jana (Jumanne) kwa ajali ya gari wilayani
Mpwapwa.
“Tumepoteza kifaa muhimu
katika kuhamasisha michezo nchini na nifikishieni salamu zangu za
rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu na wanamichezo wote
nchini”, Dk. Mwakyembe amesema na kuwatakia BMT mafanikio katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Imetolewa na:
Tags
MICHEZO