
KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amewatoa hofu
mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa timu itaimarika na kupata matokeo
bora msimu ujao.
Kauli hiyo imekuja saa chache
mara baada ya kikosi hicho kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji,
kwenye mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao uliofanyika Uwanja
wa Amani, Makambako jana jioni.
Kocha huyo raia wa Romania
alibadilisha kikosi chote kilichocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya
City isipokuwa beki David Mwantika, kilichosheheni wachezaji wengi wapya
vijana kabla ya kipindi cha pili kuabadilisha tena kwa kukiingiza
kikosi kingine cha wachezaji wakongwe.
“Ligi ya hapa inaanza baada ya
mwezi mmoja na mashabiki wanatakiwa kuelewa ya kuwa matokeo haya
hayamaanishi chochote, bado tupo kwenye kipindi cha maandalizi na timu
itafanya vizuri msimu ujao cha muhimu ni mshabiki kuendelea kuisapoti
timu,” alisema Cioaba wakati akizungumza na mtandao wa klabuwww.azamfc.co.tz
Alisema aliwatumia kikosi
kingine cha wachezaji vijana katika mchezo huo ili kuwafahamu wachezaji
wake na watu kujonea Azam FC inatarajia kuvuna nini kwa siku za baadaye,
kama mikakati aliyojiwekea katika mechi za Nyanda za Juu Kusini
“Leo (jana) nilifanya mabadiliko
kwa kuwachezesha wachezaji vijana waliopandishwa na baadhi ya wachezaji
wapya, ili kuona kitu gani kinaweza kutokea hapo baadaye, kuona viwango
vyao, wengi walizoea kucheza kwenye kiwanja cha nyasi bandia pale Azam
Complex, hawakuwahi kucheza katika kiwanja kama hiki.
“Kama kocha nimejaribu kuwatumia
wachezaji wote niliokuwa nao hapa, nikisharejea Chamazi baada ya mechi
hizi nitapitisha orodha ya mwisho ya wachezaji wangu wa msimu ujao,”
alisema.
Alisema: “Nitaendelea programu
yangu ya mazoezi huku na sitaangalia matokeo baada ya kurejea nyumbani
na wachezaji wote wa timu ya Taifa watakaporejea na kufanya nao mazoezi
kwa pamoja, Daniel, Stephan, Himid, Mahundi, Shaaban, Mbaraka, Salmin na
wachezaji wengine wapya wawili na kuwafanyisha mazoezi ya kiufundi
pamoja na kuijenga timu, kwa mashabiki wa kweli nawapa ujumbe kuwa timu
hii itakuwa na matokeo mazuri.”
Cioaba alisema kuwa kwa sasa ni
muda wa kuwarekebisha wachezaji wote kwa ajili ya msimu ujao na kudai
mashabiki wanatakiwa kuwa na uvumilivu na kuwapa sapoti wachezaji wote
waliokuwa kwenye timu.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki
bora ya NMB na Maji safi ya Uhai yaliyokuja na muonekano mpya, leo
asubuhi imeanza safari ya kuelekea mkoani Iringa kucheza mchezo mwingine
wa kirafiki wa kuhitimisha ziara ya Nyanda za Juu Kusini, utakaofanyika
Uwanja wa Samora kesho Jumatano.
Tags
Azam fc