Na Judith Mhina – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ni kielelezo kwetu na atakumbulwa daima
na wana Chongoleani wa kizazi hiki cha sasa na kijacho.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Kijiji cha Chongoleani Bw. Mbwana Nondo alipofanya mahojiano na Idara ya
Habari MAELEZO mapema leo kwa njia ya simu.
Nondo aliendelea kumshukuru Rais
Magufuli, kwa kuleta mradi wa “Bomba la Mafuta” linalojengwa kuanzia
Hoima Uganda, mpaka Tanga katika kijiji cha Chongoleani; “Kwa kweli kwa
moyo wa dhati kabisa naomba tumshukuru sana sana Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kutujali wananchi wake
na kutuletea neema ya Mradi wa Bomba la Mafuta”.
Aidha, amesisitiza;“Katika maisha
yetu wana Chongoleani, hatutaweza kumsahau sisi tuliopo wakati huu na
vizazi vijavyo, daima atakuwa mioyoni mwetu, huyu ni shujaa kwetu. Kwa
sasa vijana wengi wamepata matumaini ya maisha yao kuwa bora na
wameahidi kujituma na kufanya kazi kwa bidii watakapopata ajira katika
mradi husika”.
Akifafanua kuhusu suala la
vijana Mwenyekiti Nondo amesema; “Wana Chongoleani hususan vijana
naomba msome kwa bidii kwa wale ambao bado wapo shule na kwa wale
walimaliza mafunzo mbalimbali, wanamategemeo makubwa Rais atawapigania
wapate ajira. Hii itakuwa kichocheo tosha kwa wale wasio penda shule au
elimu waone wivu ili wasome kwa bidii kwa kuwa, elimu ni ufunguo wa
maisha.
Vilevile, Nondo aliainisha
shughuli za kiuchumi kijijini hapo amesema; “Hapa kijijini tuna idadi ya
wavuvi kama 200, Mradi wa bomba la mafuta mpaka sasa haujaelekeza suala
lolote kwa upande wa eneo letu kubwa la uchumi ambalo ni uvuvi. Hata
hivyo, wavuvi wengi wamejiunga kwenye vikundi ambavyo wanashirikiana
katika vikoba, vikundi vina idadi ya watu 15 mpaka 20”.
“Kama viongozi bado tunaendelea
kuhamasisha wavuvi waweze kujiunga kwa kuwa kuna fedha za milioni 50
kila kijiji huenda wakanufaika na hizo. Pia, kuna ujio wa mikopo kwa
wavuvi kama ilivyoainishwa kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri wa Kilimo
Mifugo na Uvuvi Mhe Charles Kizeba”. Amesema Nondo
Amemalizia kwa kuwasihi
Watanzania, kwa kusema; “Kwa moyo mkunjufu kabisa tunawaomba Watanzania
wote wajue Mradi wa Bomba la Mafuta, ni wetu sote kwa pamoja, nina
hakika matunda ya mradi huu tutayapata wote Chongoleani ni muwakilishi
tu kati ya vile vijiji, bomba litakapopita na kwa niaba ya Watanzania
wote”. Tumpe ushirikiano Rais wetu anaitakia mema Tanzania nina hakika
tutafika mbali kimaendeleo.
Naye Mtendaji Kata wa Chongoleani
Bw Mohamed Salum amesema; Rais Magufuli ametupa zawadi kubwa sana
ambayo imeweza kuitangaza Kata ya Chongoleani kimataifa, ujio huu wa
mradi wa Bomba la Mafuta umetuletea barabara kitu ambacho ni historia
kwa wana Chongoleani.
“Wananchi wana hamasa kubwa kwa
ujio wa mradi huu, mpaka sasa kaya 256 zitahama kupisha mradi, na tayari
tuko kwenye maandalizi ya kufungua akaunti kwa wale wote watakaopisha
mradi ili walipwe mafao yao, kwa kuingiziwa benki moja kwa moja”.Amesema
Salum
Kijiji cha Chongoliani kipo
kilometa 23 kutoka Tanga mjini, kina idadi ya watu 4737 kaya 1811
wanawake 2410 wanaume 2327 vijana 1672 , Kijiji kipo pembezoni mwa
barabara ya kuelekea Mombasa.
Tags
RAIS MAGUFULI