WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya
kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.
Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatano, Julai 19, 2017) wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe Bibi
Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.
Amesema Serikali haitavumilia
kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na
badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.
“Tutashughulika na watu wote
wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao,
vyeo vyao na mamlaka walizonazo.”
Pia amewaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo
baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical Brother Hood, Rabison
Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Mheshimiwa Rais
Dkt. John Magufuli.
Amesema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.
“Rais Dkt. Magufuli amefanya
mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani
kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua
wakiwemo viongozi wa dini.”
Pia aliwaomba wananchi kufanya
maandalizi mapema kwa sababu wote ni wapitaji, hivyo waandae roho zao
kwa kuacha kufanya dhambi na maovu yote ili wawe na mwisho mwema.
Vile Vile Waziri Mkuu amewaomba
wananchi wote washirikiane kwa pamoja kumuombea Dkt. Mwakyembe na
familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki
kigumu.
“Wajibu wetu sote ni kumuomba
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. Tunajua kwa sasa
Dkt. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu, namuhakikishia kwamba hayuko
peke yake kwani Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu.”
Naye, Spika wa Bunge, Mheshimiwa
Job Ndugai alimpa pole Dkt. Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea
kuwa na upendo kama ule uliokuwepo wakati wa uhai wa marehemu Bibi
Linnah.
Kwa upande wake, Mtoto mkubwa wa
marehemu, George Mwakyembe alisema anaamini mama yao, alijiandaa na kifo
hicho kwa kuwa alikuwa mchamungu.
“Mama alikuwa na ratiba kila siku
ifikapo saa nne usiku lazima afanye ibada, Hivyo nina matumaini makubwa
kupitia Uchamungu wake, Mwenyezi Mungu atamuweka mahala pema.”
Tags
MAJALIWA