Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini
Hamoud Jumaa ,akizungumza mara baada ya waziri wa afya ,jinsia ,wazee
na watoto Ummy Mwalimu kutembelea kituo cha afya cha Mlandizi
Waziri wa afya
,jinsia,wazee na watoto Ummy Mwalimu ,akitembelea kituo cha afya
Mlandizi ,wa kwanza kushoto ni mganga mfawidhi wa kituo cha afya
Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,ambae amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi
.(Picha na Mwamvua Mwinyi )
………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WAZIRI wa afya, jinsia ,wazee na watoto ,Ummy Mwalimu
,amemsimamisha kazi mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dk.Mpola
Tamambele,kutokana na kushindwa kusimamia maelekezo ya serikali ya
kuhakikisha mama mjamzito ,mtoto chini ya miaka mitano na mzee wanapata
huduma bure .
Kutokana na kutokuwa
na mamlaka ya moja kwa moja amemuagiza kaimu mkurugenzi wa halmashauri
ya halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Beda Mmbaga kumsimamisha kazi mganga
mfawidhi huyo mara moja wakati uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili
zikiendelea .
Amemuelekeza kaimu
mkurugenzi huyo pia kuwafuatilia watumishi wa afya kituoni hapo
waliohusika kumuagiza mama aliyejifungua Salma Khalifan kwenda kununua
vifaa vya kujifungulia vya sh.180,000 ili apate huduma .
Aliyasema hayo wakati
alipokwenda kutembelea kituo cha afya Mlandizi ,kabla ya kukabidhiwa
kwa magari ya wagonjwa matatu kutoka kwa mbunge wa jimbo hilo ,Hamoud
Jumaa .
Waziri huyo alisema
yeye hana mamlaka ya moja kwa moja kumsimamisha kazi mganga mfawidhi
huyo hivyo anaiachia mamlaka husika isimamie jukumu hilo.
Alisema hatokubali kuona watumishi wachache kwenye vituo vya afya ,zahanati na hospitali wanachezea maagizo ya serikali.
Alifikia
hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mama aliyejifungua
ambae alisema amenunua vifaa vya kufanyiwa operesheni kwa gharama ya sh
.180,000 .
Ummy alisema
haiwezekani kuona mama wajawazito ,wanalipishwa hadi gloves na pamba ili
kujifungua wakati serikali yao ilishasema watahudumiwa bure .
Alieleza kwamba
,kuanzia sasa waganga wakuu wa wilaya ,mikoa na watumishi wa afya wote
nchini wahakikishe wanatimiza maelekezo ya serikali kuhudumia akinamama
wajawazito na watoto ili kupunguza vifo vya uzazi .
Ummy alisema kuwa
,watumishi na wauguzi wengi wanajituma na kufanya kazi zao kifanisi ila
wapo wachache ambao wanakwamisha juhudi hizo .
“Sitokubali mtumishi
anakwenda kinyume na serikali ,rais wetu John Magufuli anasisimamia
suala zima la kuboresha huduma za afya ,halafu akitokea mtu mmoja mzembe
anatuchanganya kwakweli sitoweza kumfumbia macho “
“Wananchi wamekuwa
waoga hata kuingia katika suala la bima ya afya kwa sababu ya mambo kama
haya ,namsimamisha mganga mfawidhi huyo hadi hapo uchunguzi
utakapokamilika .” alisema Ummy .
Mbali ya hayo Ummy
alibainisha,bajeti ya dawa katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha
imeongezeka ndani ya miaka miwili mfululizo kwenye uongozi wa serikali
ya awamu ya tano .
Ummy alisema mwaka
2015/2016 bajeti ya madawa katika halmashauri hiyo ilikuwa mil.24 na
2017 ilifikia mil.70 na bajeti ya sasa 2017/2018 imefikia sh. mil.101 .
Kwa upande wake mama
aliyejifungua kituoni hapo ,Salma Khalfani ,alimweleza Ummy kwamba
aliandikiwa orodha ya dawa za kununua kwenye maduka ya dawa ya nje .
Alieleza ,alitakiwa
kufanyiwa upasuaji na hivyo kutakiwa kununua madawa na vifaaa tiba
,pamba na gloves vya 180,000 akanunue ili aweze kujifungua .
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Mmbaga alisema maagizo aliyopewa na waziri ameyapokea na atayafanyia kazi .
Nae mbunge wa jimbo
la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaaa alisema kumekuwa na malalamiko mengi
juu ya wananchi hasa akinamama kulipishwa fedha za dawa na vifaa tiba .
Alisema baadhi ya wazee wamekuwa wakishindwa kupewa huduma za afya bila malipo .
Jumaa alimuomba Ummy kuendelea kushirikiana nae kuwadhibiti watumishi wazembe wanaodidimiza haki za wananchi .
Tags
AFYA