…………………….
MALIPO YA KODI YA ARDHI PAMOJA NA TOZO NYINGINE SASA KULIPWA KIELEKTRONIKI.
Na; ELIAFILE SOLLA
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza rasmi kutumia mfumo wa kielektroniki wa Government electronic Payment Gateway (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo nyingine zinazotokana na sekta ya ardhi nchini.
Mfumo huu utamrahisishia mwananchi
kulipa kodi ya pango la ardhi popote alipo, ikiwa ni pamoja na kulipia
tozo nyingine mbalimbali za sekta ya ardhi. Pia mfumo wa GePG,
utamuwezesha mwananchi au mmiliki wa kipande cha ardhi, kujua anadaiwa
kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia popote alipo bila
kusumbuka kufuata huduma hizo katika vituo vya makusanyo.
Majaribio ya ukusanyaji kodi ya
pango la ardhi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki yalifanywa katika
mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, baada ya mafanikio makubwa kuonekana
elimu ikatolewa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi katika Halmashauri
zote za mkoa wa Dar es salaam kabla ya zoezi hilo kuhamishiwa mikoani.
Mwananchi yeyote anayemiliki
kiwanja au shamba lililopimwa na kuwa na hati, ataweza kutumia simu yake
ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na
kukulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi pia.
Kwa zile huduma nyingine za sekta ya ardhi ambazo zinahusisha malipo kama vile upekuzi katika daftari la msajili (official serach),
mwananchi atapaswa kutembelea ofisi za Wizara ya ardhi zilizo katika
eneo lake na kupatiwa makadirio ya kulipia huduma husika pamoja na namba
ya malipo itakayomuwezesha kulipia aidha kwa njia ya benki au simu ya
mkononi.
Kwa sasa kikosi kazi kinachotoa
mafunzo juu ya matumizi ya mfumo huu kimeshaanza kuelemisha mikoa
mingine baada ya kupata mafanikio mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam.
Lengo kubwa la kutumia mfumo huu ni kuongeza ufanisi katilka ukusanyaji
wa maduhuli ya serikali pamoja na kurahisisha ulipaji kodi ya pango la
ardhi nchini,
Tags
KODI