Na.Samuel Samuel
Dirisha la usajili kwa vilabu vya
ligi kuu, ligi daraja la kwanza na la pili umefungwa rasmi tarehe 6
August 2017 kwa wachezaji wa ndani na kwa wachezaji wa nje dirisha
linafungwa kesho tarehe 15 August 2017 saa sita kamili usiku.
Vilabu 62 kati ya 64 vimekamilisha
usajili wake huku viwili vikishindwa kukamilisha usajili na kushushwa
daraja . Vilabu hivyo ni Pepsi ya Arusha na Bulyanhulu ya Shinyanga
vilivyokuwa ligi daraja la pili.
Msimu huu wa usajili 2017-18 klabu
zikiingia upya kandarasi na wachezaji waliomaliza kandarasi zao,
kusajili wapya , kuwatoa na kuwapokea kwa mkopo wengine ; ni gharama za
kifedha ndio zilikuwa zikitumika ili kufanikisha zoezi hilo. Kila klabu
imetumia kiwango cha fedha kulingana na uwezo wao, mahitaji ya aina ya
wachezaji iwatakao na malengo mama katika ligi.
Katika matumizi hayo; klabu ya
Simba SC mabingwa wa kombe la Azam Sports Federation Cup linalotoa
mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika (
CAF ) wameibuka vinara katika fungu walilolitumia kwa usajili. Simba
imetumia bilioni 1.3 kwa mgawanyo ufuatao ;
USAJILI KWA WACHEZAJI WA NDANI
Simba SC imetumia kiasi cha
milioni 360 za kitanzania kusajili wachezaji wa ndani katika kuimarisha
kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa 2017-19. Fedha hizo zilitumika
kuingia kandarasi mpya kwa wachezaji waliokuwa wamemaliza mikataba yao
na kusainisha wachezaji huru wapya .
DAU LA UHAMISHO
Usajili uliohusisha uhamisho wa mchezaji kutoka klabu nyingine umetumia kiasi cha shilingi milioni 100 za kitanzania .
USAJILI WA WAGENI
Katika kusajili wachezaji wa
kigeni kutoka nje , klabu hiyo ya pili kwa ukongwe nchini imetumia kiasi
cha shilingi milioni 453! .
Katika dirisha dogo la usajili 2016-17 fedha ambayo inaingia kwenye bajeti hii , Simba walitumia milioni 346.
Kwa ujumla bajeti hiyo inawafanya
Simba SC kutumia bilioni 1.259 za kitanzania ambazo zikiainishwa na kodi
mbalimbali na matumizi mengine jumla kuu inakuja bilioni 1.3 na
kuwafanya vinara wa matumizi ya fedha kwa msimu huu.
Simba SC kwa mujibu wa taarifa ya
muhasibu mkuu wa klabu hiyo , makusanyo ya klabu hiyo kwa mwaka ni
bilioni 1.6 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kama ifuatavyo hapa
chini.
Haki za matangazo ya Runinga ( Azam media )
Katika udhamini huu wa Azam TV
Simba SC wanakusanya kiasi cha shilingi milioni 184 kwa mwaka . Dau la
kawaida la milioni 123 la udhamini kwa vilabu vyote na fedha za Simba
TV.
Mdhamini mkuu wa ligi kuu ( Vodacom )
Kampuni ya Vodacom ambao ni
wadhamini wakuu wa ligi kuu nchini, wanatoa kiasi cha milioni 108 kwa
mwaka sawa na shilingi milioni 9 kwa mwezi .
Diamond Trust Bank wadhamini shirikishi wa ligi kuu nchini wanatoa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa mwaka .
Mdhamini mkuu wa klabu ( Sportpesa )
Udhamini huu ni mpya kwa klabu ya
Simba ambao umeingiwa mwezi juni mwaka huu na unaipatia klabu hiyo
milioni 990 za kitanzania kwa mwaka . Ni kandarasi ya miaka mitano.
Jumla kuu katika mapato haya ni
bilioni 1.607 kwa klabu ya Simba. Hili ndio kusanyo lao kuu kwa mwaka
katika bajeti yao ya 1.3 bilioni ikiwa na maana kiasi kinachobaki ni
milioni 270 mpaka 300 kama faida kwa klabu. Fedha ambayo ndio inaingia
katika bajeti ya maendeleo ya klabu.
Kiuchumi bajeti kuu ya klabu ya
Simba kwa ujumla wake kwa mwaka katika matumizi ya kawaida tu ya klabu
ni 1.5 bilioni ukiondoa mipango ya kimaendeleo katika kuipa klabu hiyo
nguvu za kiuchumi.
Tuanze kuitazama Simba SC katika hii mizani na aina ya soka tulilonalo.
Hatuwezi asilani kubeza matumizi
ya klabu hiyo kulingana na mfumo wa soka ulivyo hivi sasa duniani. Soka
linasimama katika muhimili wa uchumi wa dunia kwa maana ya pesa. Pasipo
na pesa hakuna maendeleo ya soka bali penye pesa ndipo ua la pesa
linachanua vyema.
Matumizi haya tunayaona makubwa
yasiyo na tija kulingana na uwekezaji wetu mbovu katika soka katika
nyanja zote ila katika ulimwengu wa soka bado ni matumizi madogo sana.
Kwanza kabisa vilabu vyetu ikiwemo
Simba havina mifumo bora ya kiuchumi kutanua misuli yao kiuchumi .
Endapo hili lingekuwa bora hii bajeti isingekuwa habari kuu mtaani kwa
sasa . Klabu kama ingekuwa na soko zuri la bidhaa zake , miundo mbinu
bora ya soka na mafanikio mazuri uwanjani kwa maana ya kushinda vikombe
vikubwa barani Africa au kufika mbali katika hilo ambapo mamilioni ya
dola hutolewa , watu wasingehoji kwanini Simba, Yanga au Azam wanatumia
kiasi hicho cha fedha.
Simba wanaweza kujitetea
wamewekeza kiasi hiki kikubwa cha fedha kwakuwa baada ya misimu minne
sasa ndio wamepata fursa ya kuiwakilisha nchi kimataifa hivyo wanahitaji
uwekezaji mzuri katika masuala ya kiufundi kwa maana ya kusajili
wachezaji wazuri ( quality players ) ili wafike mbali kwenye kombe la
Shirikisho na kujichotea mamilioni ya CAF pia kushinda vikombe vya
ndani.
Wadhamini wa ligi kuu Vodacom
ambao wanatoa milioni 108 kwa mwaka sawa na milioni 9 kwa mwezi hawa
ndio wanaweza kukufanya ushituke na bajeti ya Simba SC ya bilioni 1.3.
Ni lazima wadhamini waangalie matumizi ya vilabu hivi na angalau na wao
udhamini wao uwe theluthi ya matumizi yao kwa mwaka ili kuvipa nguvu
kifedha ili uwekezaji mwingine nje ya uwanjani ufanyike kwa maana ya
miundo mbinu bora kisoka ; viwanja vikuu na vya mazoezi.
Bajeti hii hatuwezi kuihukumu hivi
sasa bali mwisho wa msimu ndio tutaweza kuwanyooshea vidole Simba SC
kwanini walitumia bilioni 1.3 pasipo kufikia malengo yao ? Bajeti hii
ikiishiwa kuwapa kombe la ASFC lenye thamani ya milioni 50 ni hasara kuu
pia likiishia kuwapa kombe la ligi kuu lenye thamani ya milioni 84 bado
ni hasara. Kufika mbali katika michuano ya kombe la Shirikisho hususani
kuvuka hatua ya makundi ndio faida pekee. Kwanza watapata zaidi ya
milioni 400 za CAF pia kujitangaza kimataifa na huenda wakapata faida ya
kuongeza wadhamini na kuuza wachezaji. Uimara wa klabu utaongeza
ushawishi kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kuingia uwanjani na
kuongeza mapato kwenye gate collection pia uuzwaji wa jezi zao endapo
mfumo utawekwa vizuri.
Kama taifa kabla ya kuiponda
bajeti ya Simba tuwaombe viongozi wapya wa TFF wawatazame wadhamini
wakuu wa ligi kwa maana ya kuongeza fedha kwenye ligi ili kuipa thamani
ligi yetu. Mathalani bingwa wa ligi kuu atoke na milioni 300! pia fedha
ya udhamini iongezeke kutoka 108 milioni kwa mwaka mpaka milioni 200 kwa
mwaka ili vilabu viweze kushiriki kikamilifu kutokana na msuli mzuri
kiuchumi. Viongozi waangalie namna ya kuongeza wadhamini kwenye ligi ili
kuwasaidia Vodacom, DTB na Azam .
Bado klabu zinapokea kiasi kidogo
cha haki za matangazo kulinganisha na faida mdhamini anayopata kwa
kurusha matangaz ya mpira ligi kuu. 123 milioni kwa mwaka bado ni ndogo
sana . Angalau apande milioni 220 kwa msimu ili vilabu vivune jasho lao
kwa haki.
Tukifanya hivyo na klabu hizi
zikajijenga vyema kiuchumi , hatutashangaa tena bajeti 1.3 ya usajili
kwa klabu inauoingiza 1.6 bilioni kwa mwaka. Vilabu vitakuwa na pato
kubwa na matumizi madogo yenye tija . Pia timu zitakuwa imara kufika
mbali katika michuano ya CAF na mwisho wa siku kuwa na timu bora za
taifa kwa ngazi zote.
Tags
SIMBA SC