Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la Polisi Mkoani Pwani ,linamshikilia
mfanyabiashara anaedaiwa kuwasafirisha wahamiaji haramu 72 raia kutoka
nchini Ethiopia,Rajabu Hitaji (30)mkazi wa Vigwaza ,Bagamoyo .
Aidha jeshi hilo linawashikilia pia wahamiaji haramu hao kwa kosa la kuingia nchini bila kibali .
Akitolea ufafanuzi
juu ya tukio hilo ,kamanda wa Polisi mkoani Pwani(ACP) Jonathan Shanna
,alisema uchunguzi unaendelea na watafikishwa ofisi za uhamiaji kwa
hatua nyingine stahiki.
Alieleza ,mtuhumiwa
Hitaji ambae ni mfanyabiashara alikamatwa jana, saa 3.30 asubuhi huko
maeneo ya pori la ranchi ya Taifa Narco ,Vigwaza wilaya ya kipolisi
Chalinze .
“Kufuatia msako mkali
ulioendeshwa na makachero wetu baada ya kupata taarifa juu ya uwepo wa
raia walioingia nchini pasipo kufuata taratibu za uhamiaji na raia hao
baada ya kugundua kuna gari la polisi linawafuatilia “
“Waliingia kwenye
hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha lakini askari wetu waliweza kubaini
mahali walipo kufuatia msako mkali uliokuwa ukiendeshwa katika ranchi
hiyo ” alisema kamanda Shanna .
Alisema askari hao walifanikiwa kuwakamata kundi la kwanza la wahamiaji haramu 63 wakiwa mahali ambapo gari halifikiki .
Kamanda Shanna
,alielezea kwamba ,licha ya kukamatwa kundi hilo askari waliendelea na
msako na kufanikiwa kukamata kundi jingine la wahamiaji haramu Tisa
,waliokuwa wakitafuta njia ya kutoroka katika ranchi ya taifa ya Narco .
Wakati huo huo ,MTU mmoja na watoto wawili wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvuka mto Ruvu kuzama.
Mtumbwi huo walikuwa
wakiutumia kutoka upande wa Vigwaza kwenda upande wa Mlandizi katika mto
huo wilaya ya kipolisi Chalinze Mkoani Pwani.
Kamanda Shanna alisema ,tukio hilo limetokea majira ya saa kumi alfariji usiku wa kuamkia agost 6.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Sikuzani Mussa(41)ambae mwili wake bado haujapatikana na jitihada za kuutafuta zinaendelea.
Kamanda Shanna,
alisema watoto waliopoteza maisha kwenye tukio hilo ni pamoja na Nusurat
Haji mwenye miezi minne na Fesali Hamza mwenye mwaka mmoja .
Aidha katika tukio hilo watu wawili waliweza kuokolewa wakiwa hai ambao ni Zuwena Ramadhani (29)na Tero Mziray (20).
“Dereva wa mtumbwi huo haijajulikana alipo na inaaminika ya kwamba yeye hajafa maji .”alisema .
Kamanda Shanna,
alieleza chanzo cha mtumbwi huo kuzama maji bado kinachunguzwa na miili
ya marehemu imeshafanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa
ajili ya mazishi .
Tags
WAHAMIAJI HARAMU